Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama kimesherehekea miaka 49 ya kuzaliwa kwa kufanya ziara ya kijamii katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambapo kiliwatembelea wagonjwa na kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo sabuni za kuogea na kufulia, vinywaji, nepi na vifaa vingine vya msingi kwa wagonjwa na wazazi waliolazwa wodini.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Julius Lugobi, amesema maadhimisho ya miaka 49 yamechaguliwa kufanyika kwa vitendo vya kijamii ili kuendeleza falsafa ya chama ya kuwahudumia wananchi.
“CCM ni chama cha watu, kuadhimisha miaka bila kugusa maisha ya wananchi kusingekuwa na maana. Tumefurahishwa sana na huduma bora zinazotolewa hapa hospitalini, hasa katika wodi ya wazazi, na hata suala la usafiri wa wagonjwa ni la kuridhisha,” amesema Lugobi.
Ameongeza kuwa mazingira ya hospitali ni rafiki kwa wagonjwa kiasi kwamba hata chakula kikianguka mgonjwa anaweza kukila bila hofu, jambo linaloonyesha usafi na utunzaji mzuri wa miundombinu.
Diwani wa Kata ya Malunga, Ahmed Haruna, ameeleza kuwa ziara hiyo ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani ya CCM inayosisitiza kuboresha huduma za afya. Alijivunia kuona hospitali ikitoa huduma bora na kuahidi kushirikiana na serikali kutatua changamoto zilizopo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Manispaa ya Kahama, Dk. Laizer Philipo, ameishukuru CCM kwa msaada huo na kutambua juhudi za wahudumu wa afya, akisema msaada huo utawapa faraja wagonjwa na kuwahamasisha watumishi wa afya.
Dk. Philipo amebainisha kuwa hospitali hiyo imekuwa kama hospitali ya wilaya kwa kupokea wagonjwa wengi kutoka halmashauri jirani, na kwamba kuwepo kwa vituo vya afya katika baadhi ya kata na zahanati kumechangia kupunguza msongamano wa wagonjwa kwani wengi wanapata huduma katika maeneo hayo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED