Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Njombe limepitisha rasimu ya bajeti ya Sh. bilioni 53 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Fedha hizo zitatumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na uendeshaji wa halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho baada ya kupitishwa kwa bajeti, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Erasto Mpete, amesema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kuimarisha shughuli za uwekezaji.
Amesema pia zitatumika kuongeza na kuimarisha mapato ya halmashauri, pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuhakikisha halmashauri inajitegemea zaidi kifedha.
Amebainisha kuwa bajeti hiyo pia italenga kuimarisha utendaji kazi wa watumishi, kukamilisha viporo vyote vya miradi ya maendeleo, pamoja na kutekeleza miradi mipya ikiwemo ujenzi wa hosteli katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) – Tawi la Njombe, kwa lengo la kuboresha mazingira ya elimu na makazi kwa wanafunzi.
Aidha, amewataka wataalamu wa halmashauri kuendelea kuongeza juhudi katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, akisisitiza kuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo sekta za afya na elimu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED