Mahakama yaamuru Jerry Silaa kulipa fidia ya bil. 3.18/-

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:21 PM Feb 03 2026
Mahakama yaamuru Jerry Silaa  kulipa fidia ya bil. 3.18/-
Picha: Mtandao
Mahakama yaamuru Jerry Silaa kulipa fidia ya bil. 3.18/-

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, imewaamuru aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Manispaa ya Kinondoni na Naomi Raymond Kwayu kulipa fidia ya Sh bilioni 3.18 kwa kubomoa nyumba ya makazi kinyume cha sheria.

Mbali na fidia hiyo, Mahakama imewaagiza wadaiwa hao kulipa fidia ya madhara ya Sh milioni 40 pamoja na gharama zote za kesi.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi ya ardhi namba 000032646 ya mwaka 2024, shauri hilo linatokana na tukio la Februari 29, 2024, ambapo Silaa, akiwa Waziri wa Ardhi wakati huo, alisimamia ubomoaji wa nyumba hiyo iliyopo Mbezi Medium Density, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Hukumu hiyo ilitolewa Januari 21, 2026 na Jaji Sharmila Sarwatt, aliyebatilisha uamuzi wa Waziri wa Ardhi wa kubomoa jengo hilo kutokana na mgogoro wa umiliki wa kiwanja namba 484 (2196), Block H.

Kesi hiyo ilifunguliwa na mfanyabiashara Johnsen Leonard Mahururu, aliyedai kuwa mmiliki halali wa kiwanja hicho na kuomba Mahakama itamke haki yake ya umiliki pamoja na kutoa zuio kwa Naomi Kwayu kuingia au kufanya shughuli zozote katika eneo hilo.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Kamishna wa Ardhi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Juma Rajab Kapungu.

Mahururu pia aliomba Mahakama ibatilishe hati ya umiliki iliyotolewa kwa Naomi Raymond Kwayu, anayejulikana pia kama Fainess Dawson Kiwia, akisisitiza kuwa ilitolewa kinyume cha sheria.

Awali, mlalamikaji alikuwa akiomba kulipwa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 16.2 kama thamani ya mali zilizoharibiwa wakati wa ubomoaji, lakini Mahakama ilipunguza kiwango hicho na kuamuru alipewe Sh bilioni 3.18 kama fidia ya nyumba iliyobomolewa.

Mahakama pia ilikataa madai mengine ya fidia ya kila siku na riba kama yalivyoombwa na mlalamikaji.