Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Samuel Malecela, amekemea vikali tabia ya kuwatukana Viongozi wa Dini, akieleza kuwa ni kitendo cha kukosa adabu, maadili na ustaarabu ambacho hakipaswi kuvumiliwa katika jamii.
Malecela amesema hakuna sababu wala kisingizio chochote kinachoweza kuhalalisha matusi dhidi ya Viongozi wa Dini, akisisitiza kuwa tofauti za maoni hazimpi mtu haki ya kufokea, kudhalilisha au kuwavunjia heshima watu wanaoheshimika katika jamii.
Akizungumza kwa msisitizo, Malecela amewataka watu wanaojiita Makada kuacha kuvaa mashati ya kijani na kuwadhalilisha wenzao wakidhani hawatasemwa, akibainisha wazi kuwa hatounga mkono tabia hiyo hata kidogo.
“Hao wanaojiita Makada wasivae mashati ya kijani wakatudhalilisha wenzao wakidhani hatutasema; kutukana Viongozi wa Dini siungi mkono kabisa,” amesema Malecela.
Aidha, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya kuwatukana Viongozi wa Dini, bado hakuna msimamo wa wazi wa pamoja wa kukemea tabia hiyo, jambo linalochochea mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Ameongeza kuwa iwapo kuna hoja au jambo la kuwasilisha kwa Viongozi wa Dini, njia sahihi ni kufanya mazungumzo kwa staha, heshima na busara, badala ya matusi au kejeli.
“Kama pana mahali pa kuomba mazungumzo nao, si kuwafokea. Kama huna adabu kutoka kwenu, endelea na tabia yako, lakini usituchanganye wote,” amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED