Wananachi wa Kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro wameiomba serikali kuharakisha kukamilika kwa mradi wa kusambaza mabomba ya maji kwenye eneo hilo, ili waondokane na kero ya ukosefu wa maji.
Walieleza hayo leo Februari 3 wakati Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro ilipotembelea miradi ya maji.
Wakizungumza na Nipashe, mmoja wa wananchi hao, Farida Mangube amesema wanaishi jirani na Bwawa la Mindu kwa miaka mingi lakini jambo la kushangaza wanakosa maji, hali inayowalazimu kutumia maji ya visima na chemchemu.
"Tatizo la maji ni la muda mrefu na sisi Mindu tumeanza kuona wakitandika mabomba ya maji tangu Oktoba mwaka jana lakini mpaka leo bado mabomba bado yapo juu," anasema.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Sais Kejo anasema tayari wameshaanza kusambaza mabomba kilometa 13.5 kutoka Mto Katiwa hadi katika katika mitaa mitatu ya Kata ya Mindu.
Aliitaja mitaa hiyo ni Madaganya, Mkwajuni na Mikoroshini ambayo haikuwa na huduma za maji kabisa.
Hivyo, amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu sababu kazi hiyo imefikia asilimia 44, inatarajia kukamilishwa mwishoni mwa mwaka huu.
Aidha, ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa wa Sh. bilioni 1.8 na kufanya wakazi 1,900 kupata huduma za maji katika kata zilizokosa maji kwa muda mrefu.
Kejo anasema kupitia mradi huo tayari mabomba yenye urefu wa kilometa 198 yameshaunganishwa na awamu ya pili wanatarajia kuunganisha mabomba yenye urefu wa kilometa 268.
Amesema awamu ya tatu wanatarajia kutafuta fedha kwa wadau za kuweka kilometa 248 za mabomba ya maji na kumaliza changamoto ya ukosefu wa maji katika kata hizo.
Anasema hali ya upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Morogoro imeimarika ambapo kwa sasa maji yanapatikana, ambapo kwenye Bwawa la Mindu linazalisha lita milioni 30 kwa wastani kwa siku kwa sasa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Elibariki Mmassy anasema wanajipanga kuwekeza katika kuvumbua vyanzo vya maji vipya ikiwemo ujenzi wa mabwawa na utafiti wa maji chini ya ardhi, ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji mkoani hapa.
Aidha, ameipongeza serikali kwa kuanzisha uwekezaji mkubwa wa Bwawa la Kidunda ambalo ni muhimii wa upatikanaji wa maji ambalo limekuwa ni kilio toka miaka 1960.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji wa Maji Vijijini (RUWASA), Sospeter Lutonja anasema wanaendelea na miradi 42 ya maji mkoani Morogoro yenye thamani ya Sh. bilioni 110.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Josephat Masunga amewataka wanaochimba madini jirani na vyanzo vya maji eneo la Mindu na Ruvu kuacha mara moja.
Anasema hiyo itasaidia suala la utunzaji wa vyanzo vya maji kupewa kipaumbele ili kuwa na uhakika wa huduma ya maji endelevu.
Masunga anasema wapo watu wanaendesha shughuli za uchimbaji madini katika vyanzo vya maji vya Mindu na Ruvu ambao bado hawajachukuliwa hatua zozote hadi sasa.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED