Serikali yapigilia 'msumari' huduma wajawazito, watoto

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 02:57 PM Feb 03 2026
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi.

Serikali imesisitiza kuwa huduma za afya kwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano zinaendelea kutolewa bure.

Imesema hiyo ni kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007, kwamba vitendo vya kutoza gharama kwa makundi hayo haviruhusiwi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi, ameeleza hayo leo Februari 3 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukonga (ACT-Wazalendo), Bakari Shingo.

Shingo alitaka kujua iwapo serikali ina mpango wa kukemea vitendo vya kutoza gharama za matibabu kwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Akijibu swali hilo, Dk. Samizi amesema Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inaelekeza wazi utoaji wa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum yakiwemo wajawazito, watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wazee.

Ameongeza kuwa serikali imeshatangaza kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) awamu ya kwanza, itakayohusisha makundi maalum ya wananchi wakiwemo watoto, wajawazito, watu wenye ulemavu na wazee.

Amesema gharama za bima kwa makundi hayo zitagharamiwa na serikali.

Dk. Samizi amesema kukamilika kwa hatua hiyo kutawezesha wazee wasio na uwezo pamoja na makundi mengine yaliyoainishwa kupata huduma za afya kwa kugharamiwa na serikali, hivyo kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.

Ametoa rai kwa waganga wakuu wa mikoa na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo ya serikali, ili wananchi wapate huduma za afya stahiki bila vikwazo.