DC Ludewa akoshwa utendaji wa mahakama

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 01:04 PM Feb 03 2026
news
Picha Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe Olivanus Thomas.

MKUU wa Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe Olivanus Thomas amesema utendaji kazi Mahakama ya Wilaya hiyo umeondoa hali ya ofisi yake kugeuka mahakama isiyo rasmi.

Amesema mahakama inaposhindwa kutenda haki ofisi ya Mkuu wa Wilaya huweza kugeuka kuwa mahakama isiyo rasmi jambo ambalo kwa Wilaya ya Ludewa imekuwa tofauti.

"Kuna maeneo mengine wananchi baada ya hukumu kutolewa bado hawaridhishwi na maamuzi hayo na hivyo kujikuta wakirejea kwa viongozi wa utawala kutafuta haki, hali hii imekuwa tofauti na inaonyesha utendaji mzuri unaofanywa na Mahakama ya Wilaya yetu," amesema.

Amesema mahakama hiyo ni miongoni mwa zinazofanya kazi kwa ufanisi kwakuwa wananchi wanaridhishwa na maamuzi yake.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini, Olivanus amesema uzoefu wake wa uongozi unadhihirisha wazi kuwa Mahakama ya Ludewa ina utofauti wa kiutendaji huku akibainisha kwamba tangu awasili katika wilaya hiyo hajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi yanayotokana na maamuzi ya mahakama hiyo.

Amesema kwa Wilaya ya Ludewa imenufaika na jitihada hizo baada ya kupatikana kwa jengo jipya la kisasa la mahakama lililopo Manda, lenye mifumo ya kidijitali na watumishi waliokwisha wasili tayari kuanza majukumu yao.