Watumishi wa Afya Shinyanga wakalia kuti kavu

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:21 PM Feb 03 2026

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amemuagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk. Nuru Yunge, kuwahamisha kwa muda daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga, Stephano Badiana, pamoja na muuguzi, Msafiri Kulwa, kufuatia tuhuma za kutoa huduma duni na kuomba rushwa kwa wagonjwa.

Ameagiza pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuingia kazini mara moja na kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya watumishi hao, kisha kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Maagizo haya yalitolewa leo Februari 3, 2026, wakati wa kikao cha viongozi na watumishi wa afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kilichofanyika katika Hospitali ya Wilaya hiyo.

Mtatiro amesema uamuzi huo umetokana na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu huduma mbovu na vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kufanywa na watumishi hao.

“Watumishi hawa wanadaiwa kutoa huduma mbovu pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa. Nimeelekeza wahamishwe kwa muda kwenda kufanya kazi maeneo mengine ili kupisha uchunguzi. Sijasema wasimamishwe kazi, bali wahamishwe kwa muda,” amesema Mtatiro.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vya rushwa na uzembe kazini, hasa katika sekta ya afya ambayo inahusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi.