Ruvuma kicheko, Sh.bilioni 69 kusambaza umeme vitongoji 634

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:45 PM Feb 03 2026
Mhandisi Deogratius Nagu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mhandisi Deogratius Nagu.

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi kabambe wa kusambaza umeme katika vitongoji 634 mkoani Ruvuma, mradi wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 69 unaotarajiwa kunufaisha wateja wa awali 20,328.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, Meneja Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu, amesema hayo Februari 02, 2026 wakati wa hafla ya kuwatambulisha wakandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed.

Wakandarasi waliotambulishwa ni Kampuni ya Energy Services Ltd, kampuni ya wazawa, pamoja na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO).

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 69,134,982,657.96 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 634 mkoani Ruvuma. Leo tumefika hapa kumtambulisha mkandarasi na maandalizi ya awali ya utekelezaji tayari yameanza,” amesema Mhandisi Nagu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Ahmed, ameipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo maono na dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na kuwataka wakandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Amesema upatikanaji wa umeme utaongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kutoa wito kwa wananchi katika maeneo ya mradi kuchangamkia fursa zitokanazo na uwepo wa umeme, kulinda miundombinu pamoja na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi.

“Mkoa una wataalam walioko tayari kufanya kazi muda wowote. Tunawahakikishia ushirikiano wa kutosha, ulinzi na usalama. Wakandarasi nanyi mnapaswa kuwa waadilifu na kujikagua wenyewe kwa wenyewe,” amesisitiza.

Akielezea hali ya usambazaji wa umeme mkoani Ruvuma, Mhandisi Nagu amesema vijiji vyote 551 tayari vimefikishiwa umeme, huku vitongoji 2,107 kati ya 3,691 vikiwa tayari vina umeme, na kazi ikiendelea katika vitongoji 731 vilivyobaki.

Amefafanua kuwa ETDCO atatekeleza mradi katika vitongoji 262 vya Wilaya za Mbinga na Nyasa kwa gharama ya Sh. bilioni 37.9, wakati Energy Services Ltd itatekeleza mradi katika vitongoji 372 vya Wilaya za Songea, Namtumbo na Tunduru kwa gharama ya Sh. bilioni 31.2.

Mhandisi Nagu ameongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, akibainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini vinakuwa vimefikishiwa nishati ya umeme. Amesema REA imejipanga kikamilifu kutekeleza miradi ya kimkakati ili kufikia lengo hilo.

Aidha, ameomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushirikiana na REA katika kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi pamoja na kuhamasisha uunganishaji wa umeme.

Kwa upande wao, wakandarasi wa mradi huo wameahidi kutekeleza mradi kwa uaminifu, uadilifu na uzalendo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za Serikali.