Tasnia ya usafirishaji nchini imo katika majonzi makubwa kufuatia vifo vya wafanyabiashara wawili wakongwe wa mabasi ya mikoani, Mohamed Hood na Nassor Seif maarufu kama Mzee NBS.
Wafanyabiashara hao wamefariki dunia kwa nyakati tofauti, huku kifo cha Mohamed Hood, mmiliki wa mabasi ya Hood na Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), akifariki dunia jana Februari 2, 2026, mkoani Morogoro alikokuwa akiishi. Kifo chake kimetokea katika siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake, tukio lililoacha simanzi kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na wadau wa usafirishaji.
Enzi za uhai wake, Hood alijizolea heshima na umaarufu mkubwa kupitia biashara ya usafirishaji wa abiria, ambapo kwa miaka mingi alimiliki na kuendesha kampuni ya mabasi ya Hood iliyohudumia safari za Dar es Salaam–Morogoro, Morogoro–Moshi–Arusha pamoja na maeneo mengine nchini. Baada ya mchango mkubwa katika sekta hiyo, Hood aliamua kwa hiyari kufunga kampuni yake, akiacha alama isiyofutika katika historia ya usafiri wa mabasi Tanzania.
Mbali na biashara, marehemu Hood alikuwa pia kiongozi wa kisiasa, akiwahi kushika wadhifa wa Diwani wa Kata ya Mji Mkuu katika Manispaa ya Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Uongozi wake uliakisiwa na busara, unyenyekevu na kujitolea kwa jamii.
Wakati huo huo, tasnia hiyo imepata pigo jingine kufuatia kifo cha Nassor Seif, maarufu kama Mzee NBS, mmiliki wa mabasi ya NBS, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu. Mwili wa marehemu NBS umesafirishwa kwenda mkoani Tabora kwa ajili ya maziko.
Mohamed Hood amezikwa leo mkoani Morogoro, huku maombolezo yakiendelea kwa familia za marehemu hao wawili ambao mchango wao katika sekta ya usafirishaji utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vijavyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED