TANZANIA ni moja kati ya timu ambazo zitakuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi Ndani (CHAN), Februari mwakani, lakini pia itakuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika, (AFCON) 2027.
Nchi zingine zitakazoshirikiana na Tanzania kuandaa fainali hizo mbili ni Kenya na Uganda.
Moja ya vitu ambavyo vinahitajika na vimeshaanza kufanyiwa kazi ni miundombibu ya viwanja na vitu vingine kama malazi, usafiri na mengine yanayofanana na hayo.
Tayari kuna ujenzi wa viwanja vipya, pamoja na kuvikarabati vya zamani ambavyo vitaonekana vinafaa kwa ajili ya michuano hiyo, lakini pia kutumika kwa mazoezi.
Haya yote yanafanyika kutokana na mapenzi ya michezo aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo hayafichiki.
Rais amejipambanua kuwa mpenzi wa michezo mbalimbali na hata kukubaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kuandaa fainali hizo, ni kutokana na juhudi zake.
Tukumbuke wakati wa maombi ya uenyeji kulikuwa na mataifa mengine makubwa kimpira Afrika yaliyoomba, lakini ile Rais Samia kuonekana yupo mstari wa mbele kutaka Tanzania kuwa mwenyeji, ilitosha kabisa kuonesha kuwa AFCON itakuwa salama zaidi itakapopigwa nchini, pamoja na washirika wake nchi za Kenya na Uganda.
Ikumbukwe mbali na kuwa rais, Dk. Samia pia ndiye Mwenyekiti wa chama tawala, CCM ambacho kinamiliki viwanja vingi zaidi nchini.
Hivyo, wakati rais akionekana kuwa na nia ya dhati ya kuendeleza michezo si uwanjani tu hata kwenye miundombinu, lakini baadhi ya watendaji wake hasa kwenye chama tunasikitika tukiona wanamwangusha.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, viwanja vinavyomilikiwa na CCM ndiyo mara kwa mara vinafungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kwa kutokidhi vigezo vya kutumika kwenye Ligi Kuu na kukumbushwa kuvifanyia maboresho na baadaye vinafunguliwa kabla ya kufungiwa tena.
Haya yamekuwa ni maisha ya kawaida kwenye viwanja hivi ambavyo mwisho wake haujulikani, ni lini vinaweza kuwa miongoni mwa viwanja vinavyotunzwa vema na kuweza kutumika kwa msimu mzima bila kufungiwa.
Na ikifuatiliwa utakuta mara nyingi vinaharibika kutokana na kuruhusu matamasha kufanyika eneo ambalo mpira unachezwa.
Hatukatai wala kuwapanga kwa matumizi kama hayo, lakini wasimamizi hao wangeweza kufanya hivyo bila kuathiri eneo la kuchezewa.
Viwanja vingi vya CCM vina eneo la kukimbilia, hivyo matamasha yangeweza kufanyika hapo bila mashabiki kugusa nyasi viwanjani.
Tumesikia kuwa mbali na kujengwa viwanja vipya, lakini vingine vitakarabatiwa kwa ajili ya michuano hiyo, pia vipo vitakavyokarabatiwa ili timu zitakazokuja zifanyie mazoezi wakati zipo hapa nchini.
Tunaona huu ndiyo wakati sasa wa kuvifanyia maboresho makubwa viwanja vyote ambavyo asilimia zaidi ya 90 ni vya nyasi asili, na watendaji kumuunga mkono Rais Samia kwa kuvitunza na kutoacha viharibike mara kwa mara kwa matamasha.
Lakini pia, iwapo vitapatikana viwanja vipya, vingine vikarabatiwa, na vyote vinavyomilikiwa na CCM ambavyo ni vingi zaidi nchini vitafanyiwa matengenezo makubwa, hivyo uzingatiaji utunzaji, nadhani Tanzania itakuwa moja ya nchi yenye viwanja vingi bora zaidi Afrika.
Huu ni wakati sasa kwa watendaji wote wa chama tawala na nje ya chama hicho, wote kwa pamoja kushirikiana katika utunzaji wa viwanja hivyo na si eneo la kuchezea tu, bali hata miundombinu ya viwanja hivyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED