MAENEO mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hasa yale yanayopata maji kutoka mtambo wa Ruvu Juu, kwa muda sasa yamekumbwa ya upungufu wa huduma hiyo. Si jambo la ajabu katika baadhi ya maeneo hayo kusikia vilio vya kukosa maji kwa wiki moja au zaidi.
Sababu kubwa iliyotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) takriban wiki mbili zilizopita ni kupungua kwa uzalishaji kutokana na upungufu wa maji katika Mto Ruvu ambao ndio tegemeo kubwa kwa upatikanaji wa huduma hiyo.
Kwa ujumla, taizo kama hilo hujitokeza zaidi majira ya kiangazi kutokana na kupungua kwa kina cha maji kwa kuwa mvua inakuwa imekatika, hivyo kusababisha baadhi ya mito inayoulisha Mtu Ruvu kuwa na kiasi kidogo cha maji.
Licha ya tatizo hilo, kupungua kwa maji kwenye mto huo, kunatokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo na ufugaji zinazofanyika kwenye vyanzo vya maji pamoja na uchafuzi wa mazingira.
Wakati wa uongozi wa Hayati Rais John Magufuli, tatizo hilo liliwahi kujitokeza na wananchi kuwa katika adha kubwa ya kupata huduma hiyo na serikali iliingilia kati na kupiga marufuku shughuli za kibinadamu na hatimaye wananchi wakaondokana na tatizo hilo. Pia katika serikali ya sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ilitolewa amri ya kuondolewa kwa watu wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye Mto Ruvu na maji yakarejea kama kawaida.
Mbali na makatazo yaliyotolewa na viongozi wakuu wa nchi kuhusu tatizo hilo, DAWASA pia ilisafisha baadhi ya visima katikati ya Dar es Salaam vilivyokuwa havifanyi kazi na kupunguza adha waliyokuwa nayo wananchi.
Wakati hali ya sasa ikiendelea na Wizara ya Maji kupitia Waziri wake, Juma Aweso, kuwapa wananchi matumaini kama alivyosema hivi karibuni kwamba mambo yatakuwa maziri muda si mrefu, ni muda mwafaka sasa wa DAWASA kuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha huduma ya maji inakuwa endelevu. Kwa maneno mengine, DAWASA inapaswa kuwa na mipango ya muda mrefu ya kuwezesha upatikanaji wa maji.
Miongoni mwa mipango hiyo ni kuangalia uwezekano wa kuwa na vyanzo vipya vya maji badala ya kutegemea vile vilivyopo pekee. Pia kumekuwa na taarifa kwamba mtambo wa Ruvu Juu unaotumika kuzalisha bidhaa hiyo ni wa muda mrefu, hivyo hauna ufanisi wa kutosha. Kama ni kweli DAWASA ina mpango gani wa kuhakikisha inakuwa na mtambo mpya na wa kisasa ambao utazalisha maji kwa wingi?
Aidha, kama inavyoeleweka kuwa maji ni bidhaa adimu kwa matumizi ya kila siku kwa binadamu na mamlaka hiyo inatoa huduma yenye mtazamo wa kibiashara, ni vyema ikawa na maono ya kuwa na huduma endelevu kwa kutumia teknolojia ya kuvuna maji ya mvua na kuyahifadhi.
Watendaji wa DAWASA wanapaswa kubadilika kifikra kwa kufanya kazi kisasa zaidi badala ya mazoea ya miaka nenda miaka rudi. Kama maji hupungua wakati wa kiangazi, kama ilivyo sasa, na wananchi kupata shida, watendaji wa mamlaka hiyo wachukue hatua ya kuwa na visima pia ambavyo vitasaidia kupunguza tatizo kwa wananchi.
Haiwezekani tatizo likawa linajirudia na watendaji wakawa wanajua sababu na kutoa majibu yale yale kila mwaka badala ya kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu upatikanaji wa maji. Kama ambavyo imekuwa ikielezwa kuwa sababu ni kupungua kwa maji katika Mto Ruvu ambao wakati wa masika hufurika, kwa nini kipindi hicho mamlaka isivune maji ya kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye?
Ni vyema hatua madhubuti zikachukuliwa kupunguza au kumaliza tatizo la maji katika mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo yanahudumiwa na DAWASA.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED