BUNGE la Tanzania linaendelea na mkutano wake wa 13 jijini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine, limepokea na kujadili uchanguzi wa taarifa za kamati za kudumu za bunge kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23.
Tayari Bunge limeshapokea na kujadili taarifa za Kamati za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC). Miongoni mwa mwambo yaliyojitokeza na kuonesha kuwakera zaidi wabunge ni kuendelea kuwapo kwa mashirika na taasisi za umma ambazo zinaendelea kuipatia hasara serikali.
Katika mjadala wa ripoti hizo juzi, wabunge walibainisha kuwa baadhi ya mashirika na taasisi yanajiendesha kwa ufanisi duni na kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini. Kutokana na hali hiyo, ilielezwa kuwa utegemezi wa mashirika na taasisi hizo umeongezeka kutoka Sh. bilioni 13.2 hadi bilioni 17.4.
Sababu kubwa zilizoelezwa na wabunge hao ambazo si ngeni kwa kuwa hata Msajili wa Hazina, amekuwa akieleza ni kuwapo kwa utendaji duni wa baadhi ya watendaji wakuu na maofisa waandamizi, ukosefu wa mitaji, tija ndogo na ufanisi. Sababu zingine ni kutokuwapo kwa mipango thabiti ya maendeleo na ya taasisi, uteuzi wa wajumbe wa bodi za wakurugenzi kufanyika kwa misingi ya kisiasa zaidi badala ya weledi, uwezo na taaluma pamoja na serikali kuziingilia bodi hizo katika majukumu yao.
Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo, baadhi ya wabunge waliochangia katika mjadala wa taarifa hizo za kamati walishauri serikali kuangalia wa kuyafunga, kuyafilisi au kuingia ubia na wawekezaji ili kuyaongezea ufanisi na kutengeneza faida.
Pia walishauri kwamba wanaoteuliwa kwenye uongozi wa taasisi hizo, wawe na uwezo, maarifa ya kazi wanazopewa. Kwa wajumbe wa bodi za wakurugenzi, wawe na uwezo na wasiteuliwe kwa misingi ya urafiki na kisiasa na pia wasipelekwe watu ambao ni wastaafu.
Kwa ujumla, kuendelea kuwapo kwa mashirika na taasisi za umma ambazo utendaji wao ni mbovu ni mzigo kwa serikali kwa sababu fedha hizo zingefanya shughuli zingine zingeleta matokeo chanya. Imebainika kwamba kati ya mashirika 35 ya kibiashara yaliyo chini ya serikali, 17 hayawezi kujiendesha, hivyo yanaendelea kupokea ruzuku kutoka Hazina.
Michango iliyotolewa na wabunge hao pamoja na ushauri vimeonesha dhahiri kwamba hawaridhishwi na hali ilivyo. Kwa mantiki hiyo, ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuchukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa ili kuleta ufanisi kwa mashirika na taasisi hizo.
Wakati wa mikutano ya watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi za taasisi hizo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kuwa serikali haiwezi kuyavumilia mashirika ya umma ambayo aliyaita mizigo kwa sababu kuendelea kuwapo kwao kunaongeza uzito katika kuyaendesha. Hata Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema hivi karibuni kuwa hatua zinachukuliwa ama kuyafuta au kuyaunganisha baadhi ya mashirika.
Ni wazi kwamba hilo ni zuri na ziko hatua ambazo zilichukuliwa kwa utekelezaji wa jambo hilo. Kasi inatakiwa zaidi katika kuchukua hatua hizo na dawa pekee ni Bunge kufanya mabadiliko ya Sheria ya Msajili wa Hazina ili kuipa meno kuyasimamia mashirika hayo.
Aidha, kuwapo kwa ushindani katika uteuzi wa maofisa watendaji wakuu wa taasisi hizo, kutawezesha kuwapo kwa utendaji wenye matokeo chanya badala ya hali ilivyo sasa ya watu kuteuliwa bila kujua uwezo wao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED