HIVI karibuni imeripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba kumekuwa na ongezeko la vitendo vya uporaji wa vitu mbalimbali vikiwamo simu za mkononi ma mikoba kupitia pikipiki ya abiria, maarufu bodaboda.
Uporaji huo umekuwa ukifanywa na madereva wa pikipiki hizo kwa kuvizia watu waliosimama kwenye vituo vya mabasi wakisubiri usafiri wa kwenda sehemu mbalimbali ama nyumbani, kazini au kwenye sherehe.
Wenye bodaboda hao, pia huwafuatilia kwa nyuma watu walioko kwenye mabasi ya abiria maarufu kama daladala na bajaji zinazosafirisha abiria kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Wakati wa kufanya uhalifu huo, madereva hao huwa na watu nyuma ambao huwafanya kama abiria na wanapofika sehemu husika, hupora mikoba au simu na wale wanaojaribu kuzuia kuibiwa huburuzwa na kupata majeraha sehemu mbalimbali za miili.
Kwa ujumla, vitendo hivi vimeshamiri katika maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Watu hao hupita katika barabara kubwa zenye magari mengi ya abiria. Baadhi ya wanaofanya vitendo hivyo, wanapofika kwenye vituo, hujifanya wanatafuta abiria wa kuwaunganisha na wale walioko nyuma kumbe nia yao ni kuangalia wanaotumia simu wakati huo au wenye mikoba ya kompyuta na ile ya kinamama.
Mkoani Dar es Salaam, mathalan, maeneo ambayo yameripotiwa kukithiri kwa vitendo hivyo ni Kinyerezi Mwisho, Mabibo External, Banana, barabara ya Maji Chumvi kutoka External hadi Bosnia, Riverside, Kimara, Mpakani maarufu kama Mwenge Vinyago na barabara ya Morogoro.
Vitendo hivi ni sehemu ya matukio ya uhalifu yanayoendelea katika miji na kurudisha nyuma maisha ya wananchi kama ilivyo kwa vikundi vya Komando Yosso, Tukale Wapi, Kiboko Msheli, Panya Road na Wadudu ambavyo vimekuwa tishio kwa maisha ya wanadamu na mali zao.
Kilio hicho kimesikika katika ngazi mbalimbali za jamii vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo baadhi, kama Jeshi la Polisi, vimekiri kuwapo kwa jambo hilo huku vikiwasisitiza wananchi waliokumbwa na mikasa hiyo watoe taarifa ili hatua ichukuliwe dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo.
Si kwamba vitendo hivyo havifahamiki kwenye vyombo vya usalama bali taarifa za wahusika na majina yao yako kwenye vituo mbalimbali vya polisi. Kwa mantiki hiyo, kama ni kuvikomesha ni rahisi lakini kwa sababu baadhi ya askari wasio waaminifu wananufaika navyo, inakuwa nguvu kuvikomesha, hivyo vinaendelea na uporaji na hata kugharimu maisha ya wananchi.
Jambo hilo ni dhahiri kwa sababu miaka kadhaa iliyopita, ofisa mwandamizi mstaafu wa polisi aliporwa simu yake eneo la Fire na alipotoa taarifa ndani ya muda mfupi magari ya polisi yalifika eneo hilo na kuwahadharisha vibaka kuwa simu waliyoipora ni ya mkubwa, hivyo wairudishe na siku hiyo hiyo, saa zisizozidi tatu ilipatikana.
Kutokana na ukweli huo, ni vyema Jeshi la Polisi likachukua hatua stahiki katika kutokomeza uhalifu huo kwa sababu baadhi ya wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana na hata pikipiki wanazotumia kufanya uporaji huo zinajulikana. Kwa mantiki hiyo, Jeshi la Polisi kama litadhamiria kupambana na uhalifu wa aina hiyo, matokeo chanya yanaweza kupatikana ndani ya muda mfupi.
Wahenga wanasema penye nia pana njia. Kwa msemo huo, kama kweli Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na watoa taarifa litadhamiria kukomesha vitendo hvyo, ni dhahiri kwamba haitachukua muda wahusika watafichuliwa na kutiwa mbaroni hatimaye kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Sambamba na hilo, wale wanaobainika kuhusika na vitendo hivyo, vyombo wanavyovitumia kufanikisha matukio hayo vitaifishwe ili kuwa fundisho kwa wengine.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED