Mabadiliko utendaji TANESCO yawe mfano kwa taasisi zingine

Nipashe
Published at 12:37 PM Sep 24 2024
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Picha: Mtandao
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)

WANANCHI katika maeneo mbalimbali nchini, kwa miaka mingi wamekuwa wakilalamikia utendaji usioridhisha wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Miongoni mwa malalamiko hayo ni pamoja na wateja kucheleweshewa kufungiwa umeme baada ya kuwasilisha maombi ya huduma hiyo.

Aidha, wananchi pia wamekuwa wakilalamikia watendaji wa shirika hilo kufika eneo la tukio inaporipotiwa kuwapo kwa jambo fulani kama vile hitilafu, kuharibika kwa transfoma na nyaya kuwa na matatizo kwa sababu ya kunguru kuzigonganisha. Baada ya kuripotiwa kwa tukio husika, wahusika walikuwa wakichelewa hadi wiki moja au zaidi kulishughuliki tatizo hilo. 

Mbaya zaidi, baadhi ya watumishi hao hasa mafundi, baada ya kuripotiwa kwa tukio, wamekuwa wakiwadai wateja kuwapa chochote ili wawafanyie kazi zao kwa haraka au kuwauliza kama wana usafiri wa kuwapeleka na kuwarudishac eneo la tukio. Hiyo yote ilitasfiriwa kuwa ni mazingira ya watumishi hao kuwashawishi wateja kutoa rushwa. 

Lakini katika maandiko matakatifu kuna msemo kwamba ya kale yamepita na sasa yamekuwa mapya. Hivyo ndivyo hali ilivyo sasa kwa TANESCO baada ya kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji. Hivi sasa huduma za shirika hilo zimeimarishwa kwa kiasi kikubwa na malalamiko yamepungua tofauti na ilivyokuwa zamani. 

Hayo yamo katika hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Boteko, wakati akizungumza wiki iliyopita na wananchi wa Kigoma katika hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi ya mradi wa umeme katika maporomoko ya Malagarasi ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme katika eneo la Kidahwe. 

Kwa mujibu wa Dk. Biteko, taarifa hiyo ya kuboreshwa kwa utendaji wa kazi TANESCO haikufanywa na shirika wala serikali bali taasisi inayoheshimika duniani kwamba hivi sasa mambo ndani ya taasisi hiyo ya umma ni mazuri. Kwa mantiki hiyo, shirika hilo limezaliwa upya kiutendaji na malalamiko yaliyokuwapo awali sasa ni historia. 

Pamoja na kuwapo kwa mabadiliko hayo ya kiutendaji, Dk. Biteko alisema sifa hizo zinapaswa kuongezeka kwa shirika kupandisha zaidi viwango vya kiutendaji badala ya kubweteka na kurudia hali ya zamani kama msemo kwamba mgema akisifiwa tembo hulitia maji. Kwa mantiki hiyo, Naibu Waziri Mkuu Biteko alisema aliiambia menejimenti ya TANESCO kutolewa sifa hizo badala yake waendelee kuchapa kazi kwa viwango vya juu zaidi. 

Kwa hakika, kupanda kwa viwango hivyo vya kiutendaji vilivyofanyiwa tathmini ya kimataifa, kumetokana na mipango na mikakati iliyowekwa na uongozi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ambayo inajumuisha wasomi nguli na wahandisi wabobezi katika sekta ya nishati pamoja na wataalamu wa masuala ya menejimenti. Kuwamo kwa wasomi hao wakiwamo waliowahi kuongoza taasisi nyeti na mabadiliko ya menejimenti yaliyofanyika karibuni, ni kielelezo kwamba hakuna mzaha katika utendaji.                         

Sifa linazopewa shirika hilo ambalo lina dhamana kubwa ya kuwapatia umeme kupitia kauli mbiu ya ‘Tunaayangazia Maisha Yako’, zinapaswa kuwa kigezo kwa taasisi zingine za umma zilizopewa majukumu ya kuwapatia wananchi huduma bora zikiwamo maji.  

Katika kufanya kazi na kupata sifa za kiwango cha kimataifa, hakuna miujiza bali ni kufanya kazi kwa bidii na maarifa ikiwamo kuweka mikakati endelevu katika kufikia malengo yaliyowekwa.  

Kwa suala la umeme, kwa mfano, kulikuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa suala hilo lakini sasa umefika mpaka vijijini na umewasaidia vijana kujiajiri kwa kutengeneza vitu mbalimbali. Pia katika baadhi ya maeneo TANESCO ilikuwa ikitumia majenereta kuzalisha nishati hiyo lakini sasa yameanza kuondolewa baada ya kusambazwa kwa umeme wa gridi ya taifa katika mikoa ya pembezoni kama Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera. 

Hatua hiyo iliyofikiwa na TANESCO iwe kioo kwa taasisi zinazotoa huduma kama vile maji ambazo katika maeneo mbalimbali, hasa vijijini, wananchi bado wanapata adha, hivyo kutumia muda mwingi kutafuta maji huku wakishindwa kufanya shughuli za uzalishaji mali. Kama TANESCO imeweza kwani taasisi zingine zishindwe na nini hasa sababu?