SERIKALI kwa kushirikiana na wadau, imekuwa ikiendesha kampeni ya masuala jumuishi ya kifedha kwa makundi mbalimbali ili kupanua uelewa kuhusu masuala yanayohusu sekta hiyo.
Lengo la kuwapo kwa kampeni hiyo ni kuwawezesha Watanzania kuwa na uelewa kuhusu fursa zipatikanazo katika sekta ya fedha pamoja na kuepuka madhara yanayoweza kuwapata ikiwamo kuingia katika mikopo umiza.
Mbali na kuweka uelewa mpana kuhusu masuala ya fedha ikiwamo mikopo, kampeni hiyo pia inahusu kuwajengea uwezo wananchi kuwa na nidhamu ya matumizi sahihi ya fedha kupitia uwekezaji na utunzaji wa fedha katika taasisi zilizosajiliwa zikiwamo benki.
Aidha, serikali kwa kushirikiana na wadau hao, imekuwa ikitoa elimu kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu namna ya kutumia mifuko ya uwekezaji na masoko ya mitaji katika kununua hisa, hivyo kushiriki katika uchumi wa nchi na hatimaye kujijengea ukwasi kwa maisha yajayo hasa baada ya kuhitimu elimu. Kwa kufanya hivyo, watu wa makundi mbalimbali wamejengewa uwezo na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha kwa ajili ya maendeleo yao na vizazi vyao.
Hatua hiyo ya kutoa elimu ya fedha, imesisitizwa zaidi na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwamba ni muhimu sasa ikaanzia katika ngazi ya shule ili kuwaandaa vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza juzi na washiriki wa mafunzo ya uongozi na usimamizi jumuishi na endelevu kwa wanawake yanayofanyika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwamfipa wilayani Kibaha, Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng'i Issa, alisema elimu ya fedha nchini iko chini.
Kutokana na hali hiyo, alisema ni vyema elimu ikaanzia ngazi ya shule huku akisisitiza wazazi kushiriki kuwafundisha watoto kuweka akiba wakiwa wadogo. Alisema ili kufanikisha azma hiyo, serikali inaandaa sera itakayoyajumuisha makundi mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, vijana wakiwa miongoni mwa walengwa.
Ni ukweli kwamba vijana wengi nchini, kutokana na ukosefu wa elimu ya fedha, wanakosa nidhamu pindi wanapopata fursa ya kupata nafasi za ajira. Vijana wengi mara wapatapo fedha, badala ya kuwekeza au kuzitumia kwa manufaa yao ya baadaye kwa kuwekeza au kufanya mambo ya maana, huishia kutumia kwa anasa ikiwamo ulevi. Matokeo yake, maisha yao huwa ya shida na taabu kwa sababu ya kukosa mwelekeo mzuri kimaisha hasa katika matumizi ya fedha.
Kutokana na ukweli huo, kama alivyosema aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa, Kanali Joseph Simbakalia (mstaafu), elimu kuhusu fedha inatakiwa kuenezwa kwa vijana kuanzia ngazi ya shule ili kuwaimarisha na kuwafanya kuwa imara. Simbakalia alisisitiza kwamba makuzi bora kwa vijana tangu wakiwa wadogo ndio msingi imara wa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Kauli ya kiongozi huyo ambaye ni mmoja wa wasomi na hazina kwa taifa, ni sawa na kauli kwamba nyumba bora ambayo chanzo chake ni msingi imara. Msingi mbovu husababisha kuwapo kwa nyumba mbovu, kadhalika nyumba imara chanzo chake ni msingi imara.
Ni wazi kwamba elimu ya fedha ikitolewa kuanzia ngazi ya shule itasababisha vijana wengi kuwa na uelewa kuhusu matumizi bora ya rasilimali hiyo kwa sababu watakapokuwa wakubwa na kuanza kufanya kazi au biashara, watapata nafasi ya kutumia kwa umakini ikiwamo kuwekeza katika masoko na mifuko ya fedha na dhamana.
Mfano hali ni katika familia za watu wa asili ya Kiasia ambao wengi ni wafanyabiashara, wazazi huanza kuwafundisha masuala ya fedha ikiwamo nidhamu katika matumizi wakilenga kuwafunza namna bora ya kupata mafanikio katika shughuli watakazofanya watakapoanza kujitegemea au kurithi biashara walizozikuta.
Kama wahenga wasemavyo samaki mkunje angali mbichi, suala la kutoa elimu ya fedha kwa vijana kuanzia shuleni ni mwafaka na linapaswa kuungwa mkono. Serikali inapaswa kuandaa sera ya mafunzo hayo na kuanza kutumika mapema kwa mustakabali wa taifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED