Bodi ya Ligi inalea timu kutumia milango isiyo rasmi

Nipashe
Published at 10:00 AM Nov 04 2024
Bodi ya Ligi.
Picha: Mtandao
Bodi ya Ligi.

KWA mara nyingine tena Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, imezitoza faini timu ambazo zimekuwa na tabia ya kupitia milango isiyo rasmi wakati wa kuingia uwanjani kwenye michezo yao.

Mwishoni mwa juma, Yanga ambayo kwa misimu kadhaa imekuwa ikifanya kosa hilo,  ilipigwa faini ya Sh. milioni 13, ambapo pamoja na makosa mengi, lakini lipo lile la kutumia mlango usio rasmi kuingilia uwanjani siku ya mchezo, kinyume cha kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo, ambapo kosa hilo faini yake ni Sh. milioni kumi.

Pili imetozwa faini ya Sh. milioni moja nyingine kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalumu cha kubadilishia nguo  kinyume cha kanuni ya 17:62, na kosa la tatu imetozwa pia Sh. milioni moja kutokana na kuwakilishwa na kocha mkuu pekee kwenye mkutano na wanahabari kinyume cha matakwa ya kanuni ya 17:58 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo, inayotaka aambatane na nahodha ama mchezaji mwenye ushawishi kikosini.

Hatutaki kwenda kwenye kosa la nne ambalo limefanywa na meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, katika mchezo wao dhidi ya Coastal Union na kisha kutozwa faini ya Sh. milioni moja na kumfungia michezo mitatu, badala yake tunataka kwenda kwenye kosa sugu la kutotumia mlango rasmi.

Labda tuseme Bodi ya Ligi imeruhusu mwanya huo makusudi ili kuingiza fedha zinazopatikana kwa faini, lakini kama lengo ni kukomesha inaweza kabisa.

Je, inawezekana? Ndiyo kwa sababu Bodi ya Ligi ilitupilia mbali maoni ya baadhi ya wadau wa soka wakati wa kutuma mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni za Ligi Kuu kabla ya msimu kuanza, ambayo yalipendekeza timu zinazoendeleza tabia hiyo kukatwa pointi pamoja na faini.

Adhabu inapotolewa kwa mwenye kosa na kisha akarudia kutenda kosa lile lile kila mara,  basi ujue haimgusi wala kumuumiza, badala yake inatakiwa ibadilishwe.

Timu zenye tabia hii zingekatwa angalau pointi moja tu, zisingerudia kosa hilo. Lakini pia Bodi ya Ligi inaonekana kulea jambo hili kwa kuwa hata kama si kukatwa pointi inaweza kabisa kuweka ulinzi wa kutosha wakati timu zinaingia uwanjani ili kuhakikisha zinatumia mlango rasmi.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba inafahamu kabisa muda ambao wachezaji wanatakiwa kuwasili, hivyo ingeweza kuweka walinzi wa kulinda milango yote, na mingine kuifunga kabisa, hilo lisingeweza kutokea. 

Milango yote ikifungwa kwa muda ule tu ambao timu zinatakiwa kuwa zimefika, halafu baada ya hapo ikafunguliwa, hakuna timu ambayo ingeweza kufanya hivyo, vinginevyo labda kama inaachia kwa makusudi ili kuingiza fedha kwa njia ya kutoza faini.

Ifike wakati Bodi ya Ligi ilisaidia Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kuilinda ligi hii kuwa na sifa zinazoendana na nafasi yake ya kuwa namba sita kwa ubora Afrika.

Haiwezekani ligi bora kama hii bado kuwe na timu, tena kubwa, zinapitia mlango usio rasmi na sababu kubwa hapa utagundua ni kile ambacho yenyewe Bodi ya Ligi imekuwa ikibainisha kuwa ni viashiria vya imani zinazodaiwa kuwa za kishirikina.

Tunataka kuona sasa Bodi ya Ligi ikidhibiti mambo haya ili kuiheshimisha ligi yetu, na msimu huu pia ukiwa wa mwisho, badala yake kuwekwe kanuni za kukata pointi hata moja tu sambamba na faini inazozitaka ili kukomesha vitendo hivyo.