WAHARIRI zaidi ya 50 wanachama wa Jukwaa la Wahariri (TEF), jana walipata fursa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya kupima afya zao eneo la moyo na shinikizo la damu ili waweze kujua hali zao na kuepuka vifo vya ghafla vinavyosababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
JKCI imetoa ofa hiyo ili wahariri waweze kujigundua kama wanatatizo katika eneo hilo, wajue mapema na kuanza tiba mara moja badala ya kusubiri mpaka tatizo linapokuwa kubwa na kutumia gharama kubwa kujitibu.
Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, gharama ya upusuaji wa moyo hufikia mpaka Sh. milioni 30.
Huduma hii haijaanza kwa wahariri pekee, bali imewafikiwa wananchi wengi nchini chini ya ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan, kupata huduma ya kupima bure na kuchunguzwa afya zao ili kubaini tatizo mapema.
Upimaji huu ni wa hiyari, kila mhariri anayeona umuhimu wa kwenda kupima afya yake anatumia fursa hiyo ipasavyo.
Uzuri wa kwenda kupima, unapata ushauri kutoka kwa wataalamu ambao watakuelekeza jinsi ya kwenda vizuri na mtindo wa maisha ili uweze kuepuka magonja yasiyoambukiza.
Upimaji huu huenda hatua kwa hatua, ya kwanza ni kupima shinikizo la damu, uzito na urefu ambapo mtu huchunguzwa kama anasumbuliwa na tatizo la shinikizo au sukari na baada ya hapo ataelekezwa kwa mtaalamu wa lishe.
Kama ikigundulika uzito ni mkubwa kuliko urefu wako, inaweza kuwa kisababishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo moyo, sukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine kama hayo.
Unapoonana na mtaalamu wa lishe atakuuliza utaratibu wako wa mlo kila siku na atakushauri milo ya kula kuanzia asubuhi unapoamka mpaka unapokwenda kulala, ambayo itakusaidia kupunguza uzito na kuwa katika afya njema pamoja na kufanya mazoezi.
Hatua nyingine ni kuonana na mtaalamu ambaye atakuuliza historia ya familia yako kama kuna watu wanasumbuliwa na maradhi ya sukari, shinikizo la damu ambayo mara nyingi huwa yanarithisha na utapewa ushauri jinsi ya kuepukana nayo.
Ukishapita kwenye hatua hizo ndipo unakwenda kwenye kipimo kimoja ambacho kitaeleza kama uko salama au una tatizo.
Upimaji huu ni hatua ya serikali ya kuhakikisha vituo vya kutoa huduma hiyo inafika karibu na wananchi ili waweze kuipata kwa urahisi na bila gharama.
Mtu anapopimwa na kukutwa na tatizo huunganishwa moja kwa moja hospitali ili aweze kuanzishiwa matibabu.
Kupima na kujua hali yako ya kiafya ni jambo muhimu hasa mtu unapofikia umri wa utu uzima kwa sababu unanyemelewa na magonjwa mengi.
Wengine wanasubiri mpaka wasikie maumivu ndipo wanapoamua kwenda hospitali wakati huo tatizo limeshakuwa kubwa na gharama ya matibabu pia inaongezeka.
Kuna baadhi ya watu wanapopata magonjwa na kuanguka ghafla, wanaanza kufikiria kuwa wamerogwa na kuanza kupoteza pesa kwa waganga wa kienyeji.
Jambo muhimu lingine la kujifunza, unapohisi una tatizo kwenye mwili wako, usikimbilie zahanati na kuishia kupata vidonge vya kutuliza maumivu. Tafadhali nenda kwenye hospitali zenye wataalamu sahihi ambao watakuchunguza na kukueleza tatizo lako.
Kuna waliowahi kwenda kwenye hospitali ambazo hazina wataalamu wa magonjwa ya aina hiyo na kuambiwa wana tatizo la moyo, kumbe hawana tatizo hilo.
Hivyo, ni vizuri kwenda kwenye hospitali zinazotambulika na wataalamu sahihi ambao watakufanyia uchunguzi wenye kukupa majibu sahihi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED