Wasiojulikana sasa wanavamia sanamu ya Nyerere kuibomoa!

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 09:20 AM Sep 27 2024
news
Mchoraji: Msamba
Wasiojulikana sasa wanavamia sanamu ya Nyerere kuibomoa!

NIKO nyumbani sina hili wala lile, nawaza tu uhusiano wa mkono na kinywa changu utakuwaje leo, pia nikiwaza hivyo hivyo kwa niaba ya familia, mara anaingia jirani yangu Deo Alufonsi, ambaye huwa hana la kusema, liwe jungu au ubuyu.

Namwona ana kimuhemuhe cha kutaka kuniambia jambo lililomshitua na kumshangaza, simkatizi namkaribisha, namruhusu na kumwomba amwage ujugu alionao nami nifaidike. 

Kwa lafudhi ya Kihaya, ananiambia kuna jambo limetokea Tabora na kuniuliza kama nalijua, hivyo namtaka amwage upupu hadharani nisipitwe pia na ubuyu wa siku. 

“Mutani, Wanyamwezi wameharibu huko kwao, wameangusha sanamu la mutani wangu mwingine, Bhabha wa Taifwa letu, Mwalimu Nyerere, wameondoka na shingo na kifwimbo chake, alichokuwa akitembea nacho! 

 In fwakti wamefwanya vya ajabhu.

“Yaani hawa Wanyamwezi wamekuwa na akili ya ngombe, kungangania sanamu kubwa kama lile na kuliangusha chini na kulibomowa na kuondoka na viungo vyake, kwa kweli wamefwanya vya kustaajabisha kweli!”

Namwelewa Deo na mimi nabaki kushangaa, kuwa nchi hii leo kuna mtu anaweza kubomoa sanamu la Mwalimu Nyerere kweli? Sanamu la Baba wa Taifa, mtu mwenye mchango mkubwa wa uhuru wa nchi hii, aliyeacha alama isiyofutika. 

Nikajiuliza inakuwaje sanamu la askari pale makutano ya Azikiwe na Samora liko imara na halichezewi na hata barabara ya mwendokasi inayojengwa sasa hivi haitaligusa, leo la Nyerere linaporomoshwa kama kibanda cha uganga kweli? 

Mkasa huu ni wa usiku wa Septemba 20 mwaka huu, ambao sanamu hilo lenye uzito wa kilo 600 lilivunjwa bila mtu yeyote kusikia wala kuona na kusambaratishwa. 

Yaani watu wasiojulikana sasa wamechoka watu wanaamua kuingia kwenye sanamu tena la mtu maarufu na mashuhuri wa Taifa hili, kweli?

Hii ni kasoro usiomithilika ya ulinzi wa kumbukumbu za Taifa hili. 

Anasema Mzee Harun Mbeyu, Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Tabora, kwamba ulishatolewa ushauri huko nyuma wa ulinzi wa sanamu hilo, lakini ukagonga ukuta wa masikio na kurudi. Hakuna utekelezaji!

 Kwa mshangao mkubwa, Mzee Mbeyu anakaririwa akisema: “Hapa ndipo eneo Mwalimu Nyerere alihutubia na kutoa machozi akidai uhuru kutoka kwa Wakoloni na palifanyika mkutano huo baada ya kupigwa kura tatu za uamuzi wa busara wa kumwondoa mkoloni, hivyo pana historia kubwa sana ya harakati za ukonbozi wetu.” 

Wasiojulikana hao wanafanya machozi ya Mwalimu Nyerere yawe kama ya samaki majini, yaani yatoweke hivi hivi yasiwe na kumbukumbu adhimu kama hii! Walivunja na nini? Tingatinga au nyundo za kawaida? Hakuna ajuaye wala aliyesikia kishindo cha ubomoaji! 

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha anayetoka mkoa mmoja na Mwalimu Nyerere, naye anasikika akisema: “Tunaweka mambo sawa, hapa pana historia ya ukombozi wa nchi hii na ni kielelezo na kumbukumbu muhimu, pia eneo la kujifunzia kujua harakati za Mwalimu Nyerere zilizofanyika hapa.” 

Akaahidi kuimarisha ulinzi na usalama na kuweka huduma ya umeme, kujenga majengo yote na kuimarisha miundombinu ya eneo hilo la kihistoria.  

Sijaelewa kabisa, hasa nikizingatia kauli ya Mzee Mbeyu, ambaye alisema walishashauri huko nyuma, lakini hakuna utekelezaji.

Maana yake, kulisubiriwa mvua inyeshe paonekane wapi panavuja, lakini kuvuja kwake kumesababisha madhara ya kifikra na kiimani, hasa kutokana na upendo walionao Watanzania kwa kiongozi wao aliyetangulia mbele ya haki.

Najiuliza, hivi kama Mwalimu Nyerere amesikia kuwa sanamu la kumbukumbu yake limevunjwa na kuibwa viungo, anajisikiaje huko aliko? 

Kwamba amesahaulika kiasi hiki mpaka hatua hii kuchukuliwa na wasiojulikana ambao ni kilio cha Taifa hili hivi sasa? Wametushinda, au?

Hivi kwanini viongozi wetu huwa wanasubiri la kutokea litokee ndipo wachukue hatua? Hivi kweli uongozi wa Tabora kwa maana ya serikali, haukuwa unajua uzito na umuhimu wa sanamu hili? 

Jaribuni mtakapopata fursa mwende nchi za Scandinavia mwone na kujifunza, jinsi sanamu kama hizi zinavyoheshimiwa na kulindwa kama si kutunzwa.

Wizara yetu ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inajisikiaje kusikia au kuona sanamu la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Burito limevunjwa na wavunjaji wasiojulikana na kuondoka na shingo na fimbo yake? 

Tusubiri uchunguzi. Kasinge Waitu Deo Alufonsi kwa kunifumbua macho na akili.