Uhuru na demokrasia, hekima iliyoiacha ilivyo na nafasi enzi hizi za vyama vingi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:59 AM Oct 15 2024
Mwalimu Julius Nyerere (katikati) na Joan Wicken (kushoto), aliyekuwa msaidizi wa Mwalimu na Malkia Elizabeth wa Uingereza (kulia). Wote ni marehemu.
PICHA: MTANDAO
Mwalimu Julius Nyerere (katikati) na Joan Wicken (kushoto), aliyekuwa msaidizi wa Mwalimu na Malkia Elizabeth wa Uingereza (kulia). Wote ni marehemu.

TUNAPOKUMBUKA miaka 24 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, atuache ni muhimu kutafakari hekima aliyotuachia, inayotuongoza kuelekea mafanikio.

Wiki hii taifa bado linalia likimkumbuka kiongozi wake mkuu aliyehakikishia kila raia wake anapata haki, uhuru na ulinzi wa maisha yake bila kujali dini, rangi, kabila na hata itikadi za kisiasa. Mwalimu Nyerere alikuwa ngome ya ulinzi kwa watu wengi hasa maskini na wasiojiweza.  

Leo tunaendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa sababu ya hekima na upendo alioturithisha watu wake, vitakavyodumu hadi mwisho wa nyakati. Ni muhimu wakati wote tumuenzi kwa kutafakari maono, matumaini na  matamanio yake kwanza  kiongozi, uhuru na demokrasia.  

Hekima ya Mwalimu Nyerere kwenye maeneo hayo matatu iliongozwa na imani yake kwenye aina ya demokrasia ndani ya chama kimoja inayompa kila raia nafasi ya kuwa huru kushiriki katika kujiletea maendeleo na kulindwa.

Alitamani sana Tanzania iwe na demokrasia inayowahakikishia uwepo wa haki na uhuru wa watu.  

Makala inamtafakari kuhusu sehemu ya hekima aliyotuachia katika kitabu chake cha “Binadamu na Maendeleo” alichokiandika mwaka 1967, akitoa mafundisho mahususi kuhusu umuhimu wa uongozi, uhuru na demokrasia kwa maendeleo ya watu. 

Anaeleza kuhusu umuhimu wa demokrasia ya chama kimoja inayohakikisha uhuru wa kushiriki katika maamuzi ya kidemokrasia ili kuleta maendeleo endelevu ya watu.  

 Anasema “…kuna mambo mawili muhimu katika maendeleo ya watu. Jambo la kwanza ni uongozi thabiti unaotoa elimu, la pili ni demokrasia katika maamuzi. Kwa sababu uongozi haumaanishi kuwapigia kelele na kuwashurutisha watu; kuonea watu au kikundi cha watu unaotofautiana nao; na zaidi sana haimaanishi kutoa amri kwao ili wafanye lile au hili. 

“Uongozi unamaanisha kuongea na kujadiliana na watu ili kuwaeleza na kuwaelewesha. Aidha, unamaanisha kutoa mapendekezo yanayojenga na kuwahamasisha watu kufanya kazi kwa vitendo kuhusu kile ulichowaelekeza au kuwaomba wafanye kama kiongozi wao. Uongozi unamaanisha kuwa mmoja wa wale unaowaongoza na kujitambua kuwa wewe uko sawa nao kama mtumishi wao…”

 Mwalimu katika kitabu hiki anasisitiza kuwa mamlaka ya uongozi uliyopewa hayana maana kuwanyang’anya watu mamlaka yao. “…Watu lazima wafanye maamuzi yao wenyewe kuhusu maisha yao kwa kufuata njia za kidemokrasia. Uongozi hauwezi kuchukua nafasi ya demokrasia; lazima uwe sehemu ya demokrasia. Kama uamuzi utahusu mambo ya taifa zima basi watafanya uamuzi huo kupitia halmashauri kuu na bunge…

Kama jambo lenyewe linahusu maisha yao  kwa mfano kujitolea kuhusu mradi wa maendeleo, watu wanaohusika lazima wafanye maamuzi yao kwa majadidiliano na uhuru. Hakuna namna nyingine maendeleo yanaweza kupatikana…”

Mwalimu aliamini katika kanuni za msingi za kidemokrasia zinazolinda na kuendeleza uhuru na umoja wa taifa. Kwenye demokrasia anasema msingi wa kwanza ni uhuru wa kujieleza na wa pili ni dhamu ya kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa kidemokrasia. Aliandika hivi: “…Kuna mambo mawili muhimu katika demokrasia, ukiyakosa hayo demokrasia haipo. La kwanza ni kila mtu ni lazima kusema kwa uhuru na maoni ya kila mmoja  lazima yasikilizwe. Hata kama mawazo ya mtu huyo hayapendwi kiasi gani, au walio wengi wanamdhania amepotoka, si kitu.…Kila Mtanzanzania, awe wa kijijini, mjumbe wa halmashauri ya wilaya, mbunge aweze kusema kwa uhuru bila hofu ya vitisho - ama katika mkutano ama nje ya mkutano…”

 Mwalimu pia alieleza kuhusu haki ya wachache katika demokrasia, akiandika: “…Watu  wenye mawazo tofauti hata wakiwa wachache, lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika majadiliano bila ya hofu ya kusumbuliwa, mawazo yao na yashindwe katika hoja ya majadiliano, siyo kwa vitisho na mabavu….” 

 Hajasahau haki  ya walio wengi kwenye demokrasia kwa kusema: “…Kadhalika wale walio wengi lazima wawe tayari kuyashikilia mawazo yao mpaka wale wachache waaridhike kuwa uamuzi uliofanywa kwenye  jambo lile ulikuwa sawa. Majadiliano lazima yaruhusiwe kuendelea kwa uhuru.. .

 Hekima ya Mwalimu inaendelea kuelekeza kuwa kama katika majadliano yenye usawa na kila maoni yametolewa uamuzi lazima ufikiwe na walio wengi lazima wafuatwe. Mwalimu anamalizia kwa msemo huu:  “…Maana kama vile walio wachache walivyo na haki ya kusikilizwa, wengi wanayo haki ya kufuatwa…”. 

 Msingi wa pili wa demokrasia kwa maelezo ya Mwalimu ni uwezo wa kushikilia uamuzi uliopatikana katika majadiliano ya kidemokrasia. Akisema“…Uamuzi ukishafanywa lazima ukubalike kuwa ni wa watu wote, na wote hata wale waliokuwa wakipinga  hawana budi kushiriki katika kutimiza jambo hilo…

“Aidha, walio wachache lazima waruhusiwe kutetea mabadiliko katika sheria au katika maamuzi. Lakini kwa sasa lazima watii sheria iliyopo mpaka hapo watakaofaulu kuwashawishi walio wengi  kukubali mabadiliko hayo. Bila utaratibu wa namna hiyo maendeleo ya aina yoyote  hayawezekani…” 

 Hekima ya Mwalimu Nyerere kuhusu uongozi na demokrasia inapita ufahamu wa kawaida na ni hazina inayoweza kutumulikia njia ya kusonga mbele kama taifa. Katika demokrasia ya vyama vingi tunayoitekeleza leo, hekima hii ya kutoa uhuru bila ubaguzi kwa watu kushiriki maamuzi na pia kwa viongozi kuongoza watu wakiwa watumishi wa watu, inafaa kuigwa.

Kanuni mbili muhimu alizotuachia Baba wa Taifa za uongozi, uhuru na demokrasia ambazo ni kiongozi kuwa mtumishi wa watu na siyo mnyampara, na kanuni ya pili ni kuwepo kwa uhuru binafsi wa kutoa maoni na mawazo mkutanoni au nje ya mkutano katika kujiletea maendeleo bila kubaguliwa au kutishwa kutokana na rangi, dini, kabila, chama cha kisiasa au kikundi kingine nayo ni ya muhimu kuzingatiwa.  

 Tunapotafakari hekima na mafundisho yake ni muhimu kuiruhusu alichotufundisha kutanda juu yetu na kutufunulia ufahamu, elimu na uelewa wa kuongoza taifa letu kwenda kwenye neema na heri. Ufahamu na elimu hii tunahitaji kuichambua na kuitohoa ili iendane na wakati tulio nao. 

Mwalimu Nyerere alilinda taifa letu na limestawi hadi leo. Tuendelee kumuenzi Baba yetu kwa kutafakari maoni na mafundisho yake na kuyaishi kadiri ya wakati tuliomo. 

 Mwandishi ni mbunge wa zamani wa Igunga na Kamishna wa Madini mstaafu.