Ubongo wa inzi unavyofanikisha kujifunza akili ya binadamu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:37 AM Oct 22 2024
 Inzi
Picha: Mtandao
Inzi

UMEWAHI kumfikiria mdudu mfano mende na akili yake, unadhani hana akili, ukweli ni kwamba anazo tena sana.

Mathalani, kama kuna mwanga haonekani, lakini usiku taa zikizimwa wanajaa jikoni au popote penye chakula. Ikitokea ukiingia ghafla na kuwasha taa wanafahamu pa kukimbilia na kujificha usiwaue kwa urahisi. Hiyo ni akili nyingi kwa mdudu. 

Mdudu nzi, naye ana akili, mfano kutembea juu ya kitu anachoona kinalika, kuelea juu na pia madume kuimba nyimbo za kuwavuta majike yote hayo yanafanywa na ubongo mdogo kuliko kichwa cha pini ya ofisini (office pin) wa inzi.

Ikumbukwe nzi huishi  siku 15 hadi 30 na inategemea hali ya joto na  maisha inayopitia. Ubongo mdogo lakini kazi kubwa na za kushangaza.

Wanasayansi wanaotafiti ubongo wa nzi wamegundua ulipo, umbo na mwingiliano wa kila seli moja kati ya seli 130,000 zinazouunda na viunganishi vyake milioni 50.

Mtaalamu mbobezi wa ubongo asiyehusika na utafiti huo mpya anaeleza kuwa haya ni mafanikio makubwa katika kuelewa ubongo wa binadamu au mtu kujifahamu mwenyewe.

 Dk. Gregory Jefferis wa Maabara ya Utafiti wa Kimatibabu (LMB), katika Chuo Kikuu cha Cambridge, anasema kwa sasa watu hawajui jinsi mtandao wa seli za ubongo katika vichwa vyao unavyoingiliana na kila moja.

"Kuna mwingiliano gani? Ni kwa namna gani mawimbi hutiririka kupitia mfumo unaoweza kuturuhusu kuchakata taarifa ili kutambua uso wa mtu, au kusikia sauti na kugeuza maneno na kuwa mawimbi ya umeme?

"Uchoraji wa ramani ya ubongo wa inzi utafanikisha kuelewa jinsi akili zetu wenyewe zinavyofanya kazi."

Anasema kuna chembechembe za nyuro milioni kwa milioni kwenye ubongo, zaidi ya zile za nzi aliyefanyiwa utafiti. Kwa hivyo mchoro wa ubongo wa wadudu unawezaje kusaidia wanasayansi kujifunza zaidi?

Picha ambazo wanasayansi wametoa zilichapishwa katika jarida la Nature, zinaonyesha nyuzi nyuzi mithili ya wavu.

Muundo wake ndiyo unaoshikilia ufunguo wa kuelewa jinsi kiungo hicho kidogo kinavyoweza kutekeleza kazi nyingi zenye kubwa na za kimahesabu.

 Kutengeneza kompyuta ya ukubwa wa mbegu ya nafaka yenye uwezo wa kazi kama ubongo wa nzi ni uwezo ambao sayansi ya sasa haijafikia.

Dk. Mala Murthy, mshiriki mwingine katika mradi huo, kutoka Chuo Kikuu cha Princeton, anasema picha hizo mpya zitaleta mabadiliko kwa wanasayansi wa mishipa ya fahamu-neva.

"Itasaidia watafiti wanaojaribu kuelewa jinsi ubongo wenye afya unavyofanya kazi. Katika siku zijazo tunatumai itawezekana kuelewa kile kinachotokea katika akili zetu.”

Hayo ni maoni yanayoungwa mkono na Dk. Lucia Prieto Godino, kiongozi wa timu ya utafiti wa ubongo katika Taasisi ya Francis Crick ya London, ambaye hayuko katika timu ya watafiti wa ubongo wa nzi.

"Watafiti wamegundua mfumo wa seli wa mnyoo mwenye nyuzi nyuzi 300 na funza ambaye ana 3,000, lakini kuelewa muunganiko wa seli za mdudu mwenye nyuzi nyuzi 130,000.

Ni kazi ya kiufundi ya kushangaza ambayo inafungua njia ya  kuuelewa ubongo mkubwa kama vile wa panya na labda katika miongo kadhaa ubongo wetu wenyewe.”

 ILIVYOFANYIKA  

Utafiti huo ulifanywa kwa kukata vipande vipande ubongo wa nzi na kuvipiga picha kila kimoja - vipande 7,000.

 Kisha timu ya Princeton ikatumia akili bandia kutoa maumbo na miunganisho ya nyuroni zote. Lakini akili bandia haikukamilisha kazi hiyo  na watafiti wakilazimika kurekebisha makosa zaidi ya 3,000,000 kwa mkono.

Hii yenyewe ilikuwa safari ya kiufundi, lakini kazi ilikuwa nusu tu. 

Ramani yenyewe haikuwa na maana isipokuwa kuwe na maelezo ya kazi ya kila nyuzi ya ubongo huo, anasema Dk. Philipp Schlegel, ambaye anatoka katika Maabara ya Utafiti wa Kimatibabu.

"Kuelezea nyuroni ni kama kuweka majina ya mitaa na miji, saa za kufungua namuda wa kufunga biashara, nambari za simu na maoni  kwenye ramani ya google."

Dk. Schlegel anaamini ulimwengu wa sayansi ya neva utaona mfululizo wa uvumbuzi katika miaka michache ijayo kutokana na ramani hii mpya.”

Ubongo wa mwanadamu ni mkubwa zaidi kuliko wa nzi, na bado hakuna teknolojia ya kunasa taarifa zote kuhusu nyaya zake.

Lakini watafiti wanaamini katika miaka 30 ijaya watawezekana kuuelewa ubongo wa binadamu wote.”

Ubongo wa nzi, wanasema, ni mwanzo wa ufahamu mpya, wa kina wa jinsi akili zetu wenyewe zinavyofanya kazi.

Utafiti huo umefanywa kwa ushirikiano mkubwa wa wanasayansi wa kimataifa, na umepewa jina la FlyWire Consortium.

BBC