Kilimo cha umwagiliaji kwa matone kinavyowapeleka mbele wakulima

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 11:57 AM Oct 22 2024

Ofisa ugani wa Kijiji cha Gedamar, Laizer Sulle (kulia), akimwelekeza mkulima, Fatuma Iddi, namna ya kuzingatia anapolima kisasa.
PICHA: MAULID MMBAGA
Ofisa ugani wa Kijiji cha Gedamar, Laizer Sulle (kulia), akimwelekeza mkulima, Fatuma Iddi, namna ya kuzingatia anapolima kisasa.

TEKNOLOJIA ya umwagiliaji wa matone inayohusisha kutoboa bomba matundu madogo kulingana na mimea inayohusika ili kuimwagilia maji, ni mbinu ya kisasa zaidi ya kulinda upotevu wa maji zama hizi za mabadiliko ya tabianchi.

Ni teknolojia inayotunza maji kwa sababu inadondosha maji kwenye shina pekee na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha maji kisifikie maeneo yasiyo na mazao. 

Mabadiliko ya tabianchi ni ajenda ya kidunia, kwa sababu ya kuathiri jamii na uchumi ikiwamo uzalishaji kwenye kilimo, kuongezeka ukame na uhaba wa maji vyote vikitatiza mazao na uoto wa asili.

Mradi wa maono ya mabadiliko kwenye mazao na udongo (VACS), unaoendeshwa katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma ni moja ya shughuli zinazowafunza wakulima teknolojia ya umwagiliaji wa matone. 

Taasisi ya kuendesha mifumo ya masoko ya kilimo (AMDT), inayoelimisha na kuhamasisha wakulima na wafugaji kuzalisha kisasa, ndiyo inayosimamia mradi wa VACS.

Mratibu wa tathmini na ufuatiliaji matokeo wa AMDT, Delta Shila, akizungumza na Nipashe mkoani Manyara hivi karibuni, anasema wakulima wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Dodoma  wanawaelimisha na kuwahamasisha kutumia umwagiliaji wa matone na mbegu bora.

Anafafanua kuwa juhudi hizo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wakiendeleza kilimo cha mbaazi, khoroko na kunde.

“Kuanzia Juni hadi Septemba mwaka huu, tumewafikia wakulima zaidi ya 600 wa mikoa hii, kipaumbele ni wakulima watumea teknolojia ya umwagiliaji wa matone kukabiliana na athari za  mabadiliko ya tabianchi,” anasema Shila.

Anaongeza:"Tunasisitiza matumizi ya mbegu bora ili kuongeza tija katika uzalishaji na kupata manufaa ya kile wanachokifanya.”

Anaeleza kuwa wanahamasishwa kumwagilia kwa matone ili waendelee kuzalisha hata kama siyo msimu wa mvua. 

MAFANIKIO 

Wakulima waliofikiwa na mradi huo katika mikoa hiyo minne wanaelezea mafanikio ya elimu hiyo kwenye kuzalisha mazao mbalimbali, kwa mfano;

Dodo Matambo kutoka Kijiji cha Gedamar mkoani Manyara, anazalisha magunia matano ya mikunde kwenye ekari badala ya moja alilokuwa anavuna kabla ya mafunzo ya VACS. 

Pia, anasema mavuno anayoyapata yanamsaidia kuinua uchumi wake hali inayomwezesha kuongeza wigo katika kilimo na kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji wa maisha kama kusomesha watoto na kuboresha makazi yake. 

Matambo anasema: “Awali milo miwili ilikuwa shida kwangu lakini sasa njaa naisikilizia kwa majirani, hiki kilimo kina manufaa kwasababu unavuna awamu nne mpaka tano kwa mwaka tofauti na ukulima waliokuwa wanafanya zamani.” 

Changamoto ya ukame ilisababisha kuvuna mara moja lakini umwagiliaji unawezesha kuvuna zaidi, anasema Matambo, anayetoa wito kwa wakulima wengine kuacha kuhofia gharama badala yake waachane na kilimo cha mazoea na watumie teknolojia ya umwagiliaji, mbegu za kisasa na kufuata maelekezo ya kitaalamu. 

Fatuma Iddi, ni mnufaika kutoka Gedamar, ambaye kupitia mradi wa VACS, anayajua masuala muhimu ya kuzingatia kufanikisha kilimo chenye tija  na kuvuna kwa uhakika.

 Ozinieli Benego, kutoka kikundi cha wakulima wa umwagiliaji, Mkoka mkoani Dodoma, anasema kutokana na uhaba wa maji awali walikuwa wanalima sehemu ndogo kuzalisha mazao yasiyotosheleza familia wala ziada ya kuuza. 

Anasema baada ya kukutana na AMDT wamepatiwa elimu ya namna ya kuendesha kilimo cha kisasa kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuchimbiwa visima pamoja na kuwekewa miundombinu ya sola, hatua ambayo imebadilisha mifumo ya kilimo kwa wananchi. 

“Awali tulianza kulima ekari moja mpaka tano lakini mwaka jana baada ya kupata miundombinu tunalima hadi 25, na mwaka huu kutokana na kupata mifumo ya umwagiliaji kwa matone tumeongeza eneo zaidi hadi kufikia ekari 41 kwa kuwa teknolojia hiyo inatusaidia kwenye matumizi bora ya maji,” anasema Benego. 

Anabainisha kuwa baada ya kupatiwa mafunzo na kufuata kanuni zote za uzalishaji sasa hivi wanapata mazao kuanzia kunia tano hadi nane kwa ekari, tofauti na awali kilimo cha mazoea ambako wakipata sana hazizidi gunia mbili. 

Anawashauri wakulima wengine kushiriki kilimo cha umwagiliaji kwa vile ni cha uhakika kwasababu hatua zote ikiwamo kulima, kupalilia, na mmea kupata maji zinafanyika kwa wakati na kwa usahihi.

 “Kulima kwa kutegemea mvua kuna changamoto mbili mvua kuwa kubwa na kuzidi kiwango lakini pia kupungua tofauti na kiasi kinachohitaji, unalima kwa kubahatisha.

 “Lakini kilimo cha umwagiliaji kinakupa uhakika mmea ukitaka maji unapata hata kama kuna jua kali tena  kwa wakati, hata ukaguzi wake unakuwa ni rahisi, pia ratiba ya kupalilia inakuwa ni maalum,” anasema Benego.

 Oska Mashoke, mkazi wa Kijiji cha Mikongani, mkoa wa Arusha, anasema amepata manufaa zaidi ya kujua  kuzalisha mbegu ya choroko na kwamba awali walikuwa hawajua kuwa zinachukua muda gani hadi kukomaa.

 Anasema baada ya kupatiwa elimu  ya kulima kisasa kwa mfumo wa umwagiliaji ndani ya siku 60 au miezi miwili wanaweza kuvuna, akieleza kuwa zao hilo ni mahususi kwa chakula na biashara.

 “Hizi mbegu walizotuletea ni bora na za kitaalamu tofauti na zile  tulizokuwa tunavuna zilisababisha kuwa na uzao mdogo,” anasema Mashoke na kuongeza kuwa,

Elimu waliyopatiwa kupitia mradi wa VACS imeinua uzalishaji kwa kufuata kanuni bora za kuotesha kitaalamu, kupalilia na kumwagilia wakiongeza uzalishaji kutoka gunia moja na nusu mpaka sita kwa ekari.

 SULUHU YA KUDUMU

 Katika hatua nyingine, Ofisa Kilimo wa Kijiji cha Gedamar, Laizer Sulle, anasema wanaufurahia mradi wa VACS kwasababu unatoa suluhu ya changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mvua kutokunyesha kwa wakati.

 Anasema kilimo cha umwagiliaji kwa matone kinawahakikishia wakulima usalama wa chakula, na kwamba vyakula ambavyo vilikuwa vinapatikana kwa msimu sasa vipo wakati wote kwasababu teknolojia inayotumika ni tofauti na ya kilimo cha mazoea.

 "Mfumo huu wa umwagiliaji kwa matone ukishauweka shambani unaendelea na mambo mengine, utakachotakiwa kufanya ni kufunga au kufungua maji, huku ukijua kwamba baada ya muda fulani mimea imeshapata maji ya kutosha.” Anasema Sulle.

 Mkurugenzi wa AMDT, Charles Ogutu, anasema teknolojia hiyo ya umwagiliaji itaendeleza kilimo nchini, akisisitiza kuwa sekta ya kilimo itabaki kuwa mama na kwamba inahitaji wataalamu na wadau wengi kuiendeleza.