Sekondari Jokate inavyoakisi azma ‘tokomeza ziro’ Kisarawe

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:51 AM Oct 22 2024



Mkuu wa Shule ya Jokate Mwegelo, Mariam Mpunga, akitoa neno wakati wa mahafali ya kidato cha nne 2024.
PICHA: JULIETH MKIRERI
Mkuu wa Shule ya Jokate Mwegelo, Mariam Mpunga, akitoa neno wakati wa mahafali ya kidato cha nne 2024.

WILAYA ya Kisarawe inayopatikana mkoa wa Pwani ni maarufu kwa mengi, kwanza ni kudumisha mila kuanzia kucheza ngoma hadi kula vyakula vya asili kama kasamvu kinachochanganywa na kunde pamoja ugali wa muhogo.

Pia, wakazi hawako nyuma kwenye uzalishaji mashambani ni wakulima mahiri wa mihogo, mbaazi na karibu kila nyumba ina minazi matunda yake mahsusi kuunga vyakula.

WanaKisarawe ni wapenzi wa ngoma ya unyago, wanayochezwa mabinti wakishafikia miaka 10, mila hiyo inayowagusa watoto wadogo kwa miaka mingi ilikuwa chanzo cha wasichana kukwama kielimu, hasa baada ya kupata mimba.

Mafunzo wanayopatiwa wakati wa ngoma hizo yanaelezwa kusababisha wengi wao wajiingize kwenye ngono na kupata ujauzito wakiwa bado wadogo na kulazimika kukatisha masomo.

Ikumbukwe zama hizo hakukuwa na mpango wa kurejea shuleni kuendelea na masomo yaliyokatishwa kwa sababu mbalimbali ukiwamo ujauzito.

Leo, mambo yamebadilika kutokana na kampeni zinazofanywa na serikali na mashirika ya kiraia kupinga mila zilizopitwa na wakati kama kuwacheza watoto unyago, zimeanza kuleta mabadiliko.

Jitihada zinaanza na aliyekuwa  Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo, kwa kushirikiana na Mbunge Dk. Selemani Jafo Waziri wa Viwanda na Biashara na viongozi wa wengine wanaandaa mkakati wa kujenga sekondari ya wasichana.

Inaanza kwa moto kauli mbiu ‘tokomeza zero Kisarawe”. Baada ya kujengwa Sekondari ya Wasichana ya Jokate Mwegelo, ikawa chachu ya wasichana wengi kupambana na kujiendeleza kimasomo.

Kuwapo kwa shule hiyo ambayo inachukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita kutoka maeneo mbalimbali kumeiamsha jamii inayowazunguka kuwapa kipaumbele watoto wao na kuanza kuzipa mgongo mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.

Kwasasa wazazi wengi wameanza kubadilisha utaratibu wa kuwacheza watoto wao kwa kusubiri wakihitimu elimu ya sekondari ndipo na wao wanatumia nafasi hiyo kutekeleza utamaduni huo.

Sekondari ya Jokate Mwegelo yenye  wanafunzi 930 kutoka  waanzilishi 86   mwaka 2021 imeendeleza kauli mbiu yake ya tokomeza zero kutokana na matokeo ya kidato cha pili,  cha nne na cha sita.

Mkuu wa shule hiyo, Mariam Mpunga, anaishukuru serikali kuondoa vikwazo katika shule hiyo na kuwawezesha wanafunzi kutumia muda mwingi kwenye masomo huku wakiongeza ufaulu kwenye mitihani yao.

“Shule yetu inafanya vizuri kitaaluma katika mitihani ya kidato cha pili na cha sita kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022, 2023 na 2024 katika mitihani ya kitaifa imefaulisha kwa asilimia 100 na hakuna daraja sifuri. Ni jambo linaloonyesha kaulimbiu ya tokomoza zero kwa vitendo ikidhihirika,” anasema.

Mariam anasema tangu kuanzishwa imekuwa na ongezeko la miundombinu na leo yako mabweni 10, vyumba vya madarasa 28, maktaba moja, maabara mbili, nyumba za walimu mbili jengo la utawala moja pamoja na matundu ya vyoo 30.

Anasema wanafunzi waanzilishi wa kidato cha kwanza mwaka huu watahitimu kidato cha nne, wakijiandaa kwa mtihani wa taifa utakaofanyika mwezi ujao kuonyesha walichovuna kwa kipindi cha miaka minne.

Mpunga anaeleza kwamba licha na kuwapo kwa jitihada za kutokomeza zero kama ilivyo lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo bado haijapata chanzo cha uhakika cha maji ya kutosha ikilinganishwa na ongezeko la wanafunzi.

Aidha, anaeleza kikwazo kingine katika shule hiyo mbali ya maji kuwa kukosa ni uzio kwa ajili ya usalama wa wanafunzi hasa kwa vile mazingira yake ni mapori.

Nyumba bora za walimu, maabara kulingana na ongezeko la wanafunzi pamoja na gari la shule la kuhudumia na kubeba wanafunzi na wafanyakazi yanapotokea matatizo mfano ugonjwa.

 “Vikwazo hivi vinavyoonekana sasa vilikuwa vikubwa zaidi, namshukuru Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Selemani Jafo, ambaye amekuwa bega kwa bega na sisi kuvitafutia mwarobaini tunaendelea kumwomba afanikishe kuimarisha mazingira ya kufundisha na kufundishia ili ufaulu unaongezeka.” Anasisitiza.

Khalfan Sika ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kisarawe, ndiye mgeni rasmi wa kwanza katika mahafali ya kidato cha nne katika shule hiyo akimwakilisha mwasisi Jokate Katibu Mkuu  wa Jumuiya ya Wanawake Taifa (UWT).

Akizungumza na wahitimu, wazazi na walezi wa wanafunzi anasema serikali itatatua vikwazo katika sekta ya elimu na kwamba tayari imetoa Sh. milioni 900 kumalizia bwalo, na milioni 30 kupanua maabara za shule hiyo.

Sika pia anamwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe kutenga bajeti kwa ajili ya kumaliza vikwazo vilivyoko shuleni hapo.

Ofisa Elimu Sekondari ya Kisarawe Edita Fue, anawakumbusha wazazi kuzingatia malezi bora kwa wanafunzi wahitimu elimu ya sekondari dhidi ya ukatili kijinsia na vishawishi hatarishi.

Diwani wa Halmashauri ya Kisarawe Hamis Dikupatile, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri wakati Jokate Mwegelo ikianzishwa anasema vikwazo vilivyoelezwa na mkuu wa shule hiyo vitatafutiwa ufumbuzi kwa kutengewa bajeti.

Dikupatile anasema halmashauri itapambana kuviondoa kwa kutenga bajeti ili wanafunzi wanaochaguliwa kusoma katika shule hiyo wajikite kwenye masomo zaidi na kuongeza ufaulu katika jambo analoliita la motisha kwa wasichana.

Mwanafunzi wa kidato cha nne Hadija Mrisho, anasema katika mwaka wao wa kwanza kutoa kidato cha nne kwa shule hiyo wanakwenda kuandika historia kwenye kufaulu na kudhihirisha kauli mbilu ya uanzishwaji wa shule hiyo kutokana na maandalizi mazuri waliyopata.

Mbali ya kufundishwa kwa bidii wanafunzi wa shule hiyo pia wamekuwa wakiletewa wahadhiri wa vyuo vikuu wanawake ili kuwapa uzoefu na motisha wa kufanya vizuri kwenye masomo yao na kuwaaminisha kwamba mwanamke anaweza kuwa kiongozi na kushika nafasi mbalimbali akijiamini na kusimamia malengo yake.

Kadhalika wanafanya ziara kwenye vyuo vikuu hususani cha Dar es Salaam lengo likiwa kujifunza na kujionea wanawake wanavyosoma vyuoni na waliofanikiwa kupitia elimu na namna walivyojikwamua kutoka kwenye vikwazo vya kuharibu malengo yao.