Nukuu ya Nyerere inapotumiwa kukimbia vyama, Msigwa aitaja

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:13 AM Jul 17 2024
 Rais Samia Suluhu Hassan, akimkaribisha Peter Msigwa, baada ya kukihama chama chake cha CHADEMA.
PICHA: MTANDAO
Rais Samia Suluhu Hassan, akimkaribisha Peter Msigwa, baada ya kukihama chama chake cha CHADEMA.

IMEKUWA ni kawaida kwa wanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine, hasa nyakati za uchaguzi, wengi wakihalalisha uamuzi wao na tuhuma za kutoridhishwa na baadhi ya mambo kule wanapopakokimbia.

Wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa ili mtu ajiunge na chama kwanza lazima akubaliane na itikadi au msimamo wa chama anachokitaka katika masuala yote ya msingi hususani namna ya kushika dola, usimamizi wa uchumi na rasilimali za nchi na muundo wa taasisi za umma hasa majeshi.

Wanadokeza kuhusu itikadi wakizitaja zipo zinazoamini katika mrengo wa kulia, wa kushoto, wa kati, kati kulia, kati kushoto, ujamaa na ukoministi.

Itikadi hizi zinaelezwa kuwa ndio msingi wa mwananchi kuamua kujiunga na chama kwa kuwa ndio imani yake kwa kile anachotaka kukiona kesho kwa nchi yake.

Mwanasiasa mkongwe, Thomas Ngawaiya, anasema ni vigumu kwa mwanasiasa makini kuhama kutoka chama kimoja hadi kingine kwa kuwa imani ya itikadi inambana.

“Ukiona mtu anahama chama ujue hakuna kitu kingine kinachomsumbua zaidi ya ubinafsi na wanasiasa wengi wanaangalia zaidi maslahi yao na sio kusaidia umma. Binafsi nalichukia jambo hili kwa sababu linarudisha nyuma malengo ya jamii,” anasema.

Anafafanua kuwa ubinafsi wa wanasiasa umekwamisha malengo ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

“Lengo kubwa la chama cha siasa ni kuwaletea wananchi maendeleo pale wanapopewa nafasi ya kuongoza kutokana na itikadi yake, ukifuatilia wanaohama ni kwa sababu wamekosa nafasi kwenye uchaguzi ndani ya chama au kutoteuliwa kuwania nafasi kama za urais au ubunge;”
 Anasema na kuongeza kuwa nia yake anayehama ni kuingia kwenye nafasi fulani sio kuisaidia jamii katika kile wanachoamini.

Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Moshi Vijijini akianzia NCCR-Mageuzi na kisha kuhamia TLP na sasa yuko CCM, anasema hakutaka kuhama lakini mazingira yalimlazimisha baada ya kugombana na aliyekuwa Mwenyekiti wake, marehemu Augustino Mrema, hadi kufikishana mahakamani.

“Siungi mkono kuhamahama vyama. Ni kikwazo kwa jamii ambayo inaamini pamoja na wewe kwenye itikadi, ghafla unabadilika. Ndio maana nasema kama si ubinafsi, kuhama chama ni jambo gumu kwa mtu makini,” anaongeza.

CCM SI MAMA 

Akizungumza na Nipashe, aliyewahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Peter Msigwa, ambaye karibuni amehamia CCM, anasema suala la itikadi kama msingi wa imani ndani ya chama cha siasa ni jambo jepesi linaloweza kubadilika wakati wowote.

“Kwani hukumsikia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akimwambia Kawawa CCM sio mama wala baba yake?” Itikadi sio dini wala sio imani ni jambo linaloweza kubadilika wakati wowote,” anasema.

Anaahidi kujibu swali hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari ambao hata hivyo hajaufanya.

CHADEMA Msigwa aliyoikimbia, inaamini katika itikadi ya mrengo wa kati wakati CCM alikohamia inaamini katika siasa za ujamaa na kujitegemea, japo kinachoonekana ni uelekeo wa mrengo wa kulia lakini pia kushikilia jukumu la serikali kusimamia maendeleo.

Itikadi inatafsiriwa na kutokana na mambo ambayo chama huyaamini, kuyasimamia na kuyapigania kama ajenda zake za msingi kwa wananchi na taifa kwa ujumla. 

ITIKADI CCM/CHADEMA
 Pamoja na kwamba wanasiasa nchini wanahama kutoka kila upande, vyama vya CCM na CHADEMA vinaongoza kwa makada wake kuhamia upande mwingine na wakati mwingine kuunda vyama kama ilivyotokea wakati wa awamu ya nne, baadhi ya makada wa CCM walivyoasisi kuanzishwa chama cha kijamii (CCK) na msuguano ndani ya CHADEMA ulivyozaa ACT-Wazalendo miaka 10 iliyopita.

Hata hivyo, CCM inaamini katika itikadi ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilipewa nguvu ya kisera na Azimio la Arusha ambalo liliweka uchumi mikononi mwa umma.

Itikadi hiyo ilisisitiza umuhimu wa kuishi pamoja jambo lililoanzisha vijiji vya ujamaa na kuimarisha vyama vya ushirika.

Falsafa ya CCM inasisitiza kuzingatia utu, usawa na haki; inayosimamiwa na siasa safi na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wa CHADEMA, inaamini katika mrengo wa kati kikiongozwa na falsafa ya ‘nguvu na mamlaka ya umma’ au The People's Power’ katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza maamuzi, mawazo, rasilimali, uchumi na siasa ya nchi.

UFAFANUZI KIMRENGO
 
 Vyama vyenye mrengo wa kushoto vinaamini katika usawa, ushirikiano, kusaidiana na kuwasaidia wasiojiweza, uhuru wa kujitawala, haki na fursa za kisiasa na kiuchumi kwa mwanamke, mgawanyo bora wa kodi, bima za afya kwa umma sambamba na haki na usawa kwa wafanyakazi.
 
 Vyama hivi vinasikiliza na kuamini katika maslahi ya msingi ya wananchi wao, mfumo wenye usawa katika uongozi, matajiri wawasaidie masikini na athari za mabadiliko ya tabianchi.
 
 Vyama vyenye mrengo wa kushoto vipo kinyume na aina yoyote ya ukandamizaji, ubaguzi wa rangi ama unyanyasaji wa kibinadamu.
 
 Kwa upande wa mrengo wa kulia vinaamini katika utamaduni wa asili wa dola kama vile kuwa na jeshi kubwa, silaha kali na kupigana vita kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi yao, utaifa na dola kwanza na ulinzi na usalama wa dola.
 
 Vyama hivi vinaongozwa na itikadi kuwa dola linapaswa kuhakikisha linapambana na vitisho vyote vya ndani na nje ili kuhakikisha linaendelea kuwepo.
 Vyama nyingine vya mrengo wa kulia vinaamini pia kuwa nchi zinapaswa kulinda maslahi yao ya kibiashara, hata kwa kuweka vikwazo wakati fulani.
 
 Vyama vyenye mrengo huu huwa haviamini sana katika ushirikiano na hata vinapokuwa madarakani mahusiano baina ya nchi na nchi huyumba.
 

Kwa upande wa Uingereza vyama vyenye itikadi ama mrengo wa kulia ni Conservative kilichoshadidia kujitoa kwa Uingereza Umoja wa Ulaya-wakiita hatua hiyo British exit au Brexi, hatua ambayo imekuwa na changamoto nyingi kiuchumi na kijamii.

Kwa Marekani Republican kinachokusudia kumteua Donald Trump kuwa mgombea urais kinaongozwa na mrengo huo na mara nyingi hakiwajali maskini wakiwamo weusi na kinaendeleza ubaguzi.

MRENGO WA KATI
 Vyama vyenye mrengo wa kati vinayaamini mambo yote yanayosimamia itikadi za mrengo wa kulia na wa kushoto kwa pamoja kwa umuhimu wake ikiamini katika ustawi wa nchi na dunia.
 
 Mfano wa vyama hivi ni chama cha Liberal Democrats cha Uingereza ingawa kuna wakati nacho huonekana kuegemea siasa za mrengo wa kulia.

CHADEMA ndicho kinachoamini katika itikadi hii kwa maana kwamba kinaangalia mambo yanayofaa kwenye mirengo yote miwili na kuyasimamia huku kikipinga baadhi ya mambo pia.


 Vyama vyenye mrengo wa kati kushoto vinaamini yale ya mrengo wa kushoto huku yale ya mrengo wa kulia wakiyakubali kwa kiasi fulani.
 
 MRENGO KATI, KULIA
 
 Kama ilivyo kwa mrengo wa kati kushoto, vyama vyenye mrengo wa kati kulia vinaamini zaidi yale ya mrengo wa kulia lakini pia huyatilia umuhimu yale ya mrengo wa kushoto.