Dk. Mpango akabidhi tuzo wasafirishaji bora na salama kwa mabasi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 05:00 PM Aug 27 2024
Dk. Mpango akabidhi tuzo wasafirishaji bora na salama kwa mabasi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Mpango akabidhi tuzo wasafirishaji bora na salama kwa mabasi.

MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amekabidhi tuzo kwa wasafirishaji bora na salama kwa mabasi ya njia ndefu huku wale wenye matukio mengi ya ajali, kuchezea mifumo ya kufuatilia mwenendo wa mabasi na kutoa huduma chini ya kiwango wakikatwa.

Tuzo hizo ambazo ziliandaliwa na  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ikiwa ni mara ya kwanza kuanza kutolewa, zilikabidhiwa katika sherehe za ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa LATRA, tuzo hizo zimetolewa kupitia shindano la kutafuta watoa huduma bora  na salama kuanzia Juni mwaka jana hadi Julai mwaka huu kwa makundi ya wasafirishaji wakubwa, wa kati na wadogo ikiwa ni sehemu ya kuchochea ushindani wenye ufanisi katika huduma za usafiri wa mabasi.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, alisema Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeipa Mamlaka hiyo wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa.

Suluo alisema utoaji wa tuzo za wasafirishaji bora na salama, ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu huo.

"Na mchujo ulifanyika kwa kuzingatia taarifa za mifumo ya LATRA ya utoaji huduma ambapo wasafirishaji wenye matukio mengi ya ajali, kuchezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi(VTS) kutoa huduma bila kuwa/kukata bima chini ya viwango stahiki, kusitishiwa leseni za usafirishaji kutokana na kutozingatia sheria na kanuni, malalamiko ya wateja kuhusu huduma zisizoridhisha, waliondolewa katika shindano,"alisema Suluo.

1
Alitaja vigezo vingine vilivyozingatiwa kuondoa baadhi ya watoa huduma katika shindano hilo kuwa ni kutowapatia abiria tiketi za kielektroni, upotevu wa mizigo ya abiria, kuzidisha nauli na makosa mengine ya aina hiyo kwa idadi inayofikia asilimia 10  ya idadi ya mabasi waliyonayo.

"Na kwa utaratibu huo idadi ya washindani ilipunguzwa hadi kubaki na washindani 15 kwa kila kundi la watoa huduma wakubwa, wa kati na wadogo.Washindani hao kwa kila kundi waliwekwa katika dodoso la kidigitali lililosambazwa kupitia tovuti ya LATRA na mitandao ya kijamii ili wadau na watumia huduma wawapigie kura, ambapo jumla ya wadau 2,237 walipiga kura kumchagua msafirishaji bora na salama,"alisema Suluo.

Suluo aliwataja washindi kundi la wasafirishaji wakubwa wenye mabasi zaidi ya 30 kuwa ni, Kampuni ya Shabiby Line mshindi wa kwanza, wa pili kampuni ya Happy Nation na mshindi wa tatu ni kampuni ya ABC Upper Class.
Kundi la pili lilikuwa la washindi wenye mabasi  kuanzia 11 hadi 30  na wa kwanza alikuwa ni kampuni ya Tilisho, ikifuatiwa na mshindi wa pili Satco Express wakati mshindi wa tatu ni Ngasere Co. Ltd.

Kwa kundi la wasafirishaji wadogo wenye mabasi matatu hadi 10, mshindi kwa kwanza ni Sama Luxury Coach, wa pili ni kampuni ya Achimwene Business na wa tatu ni RATCO Express.

"Tumeanza kutoa tuzo hizo ili kuchochea matumizi ya mifumo ya utoaji wa huduma bora na salama ya usafirishaji wa abiria kwa ufanisi na ubunifu hususani katika matumizi ya teknolojia,"alisema Suluo.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo, mwakilishi wa kampuni ya mabasi ya Tilisho Safaris, Florence Shirima,
alisema siri kubwa ya ushindi wao ni kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kutoa huduma bora kwa wateja.
2

Stella Nestory, Meneja wa kampuni ya mabasi ya Sama Luxury Coach alisema utaratibu huo wa LATRA kutoa tuzo kwa watoa huduma utachangia kuleta motisha ya kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma bora kwa wateja wao.

Katibu Mkuu Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) Priscus Joseph, aliipongeza LATRA kwa kuanzisha utoaji wa tuzo hizo kwa wasafirishaji wa mabasi ya masafa marefu na kwamba hiyo itakuwa chachu kwa wamiliki wa kampuni za mabasi kuongeza juhudi ya kazi na ubora wa huduma.

Kadhalika, katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Daniel Sillo, alikabidhi vyeti maalum vya utambuzi kwa vyama vya wasafirishaji abiria na mizigo vilivyofanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini(LATRA).

Vyama hivyo ni vile ambavyo vimechangia kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

Vyama vilivyokabidhiwa vyeti vya utambuzi ni Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania (TAMSTOA), Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT) na Chama cha Wasafirishaji Mizigo kwa Njia ya Barabara Tanzania (TRFA).

Pia, Sillo alikabidhi cheti cha utambuzi kwa Chama cha Ushirika na Mikopo cha Watoa Huduma za Bajaji za Abiria na Bodaboda Mkoani Kilimanjaro (KIBABOT SACCOS) kwa kutambua juhudi za cha hicho ambacho ni chama cha kwanza kutoa leseni za LATRA kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu kwa wanachama wao.