Mbarawa atembelea ujenzi matenki 15 TPA

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 04:47 PM Sep 13 2024
Mbarawa atembelea ujenzi matenki 15 TPA
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbarawa atembelea ujenzi matenki 15 TPA

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imeanza ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta yanayoingia nchini ambayo kukamilika kwake kutaisaidia serikali kuwa na hifadhi ya kutosha ya nishati hiyo kwa muda mrefu kuliko ilivyo sasa.

Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, aliyetembelea mradi huo wa (Oil Terminal)  unaotekelezwa Tundwi Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ujenzi huo unahusisha matenki makubwa 15 yenye uwezo wa kuhifadhi ujazo wa lita 378,000 za mafuta pindi yanapoingizwa nchini ambapo Waziri alipongeza utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika eneo la ujenzi lililopo katika kata ya Tundwi, Profesa Mbarawa, alisema kuwa ujenzi huo utakaochukua muda wa miaka miwili utasaidia sana katika kuboresha ufanisi wa bandari.

Alisema utasaidia kupunguza foleni ya meli za kupakua mafuta ambapo meli moja hutozwa wastani wa faini ya shilingi milioni 50 kwa siku moja wakati ikiwa katika foleni ya kupakua mafuta hayo.

Kwa mujibu wa Profesa Mbalawa, ufinyu wa matenki ya kuhifadhia mafuta ulisababisha wasafirishaji kutozwa kiasi kikubwa sana cha pesa na mwisho wa siku gharama hizo pia ziliwagusa wananchi.

“Wakati mwingine meli hulazimika kusubiri kupakua mafuta hata zaidi ya wiki moja, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani wasafarishaji wa mafuta wanaumia na faini hii,” alisema Profesa Mbalawa.

1

Alisema ili kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa moja ya bandari zenye ushindani duniani, Serikali imeamua kujenga matenki hayo 15 ambapo sasa meli hizo zitatumia saa chache kupakua nishati hiyo na kuondoka.

Alisema ujenzi huo utafanya kazi ya usambazaji wa mafuta hayo kwenda kwa wateja (kampuni za kuuza mafuta) kwa urahisi sana na kukabiliana na uhaba wa mafuta unaoweza kutokea.

“Nimefurahi sana kuona mradi huu hatimaye unatekelezwa na naupongeza sana uongozi wa TPA kwa hatua hii,” alisema

“Tulijaribu mara kadhaa huko nyuma lakini tulishindwa, ila mipango thabiti ya bodi na uongozi wa TPA umesababisha kutekelezwa kwa mradi huu,” alisema Profesa Mbarawa.
2

Meneja wa mradi huo, Mhandisi, Hamis Hassan Mbutu, alsema mradi huo unatarajiwa kumalizika kwa wakati na kuwa na tija kwa bandari hiyo na Serikali kwa ujumla katika kukusanya ushuru. 

Awali, akiongea kabla ya kumkaribisha Profesa Mbarawa, Mkurugenzi Msaidizi wa TPA, Juma Kijavara, alisema mkataba wa ujenzi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 678.6 ulisainiwa rasmi Februari 26, 2024 ambapo tayari Mkandarasi China Railway Major Bridge Engineering Group ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 9.9 kuanza ujenzi huo. 

Akimuelezea Profesa Mbarawa hatua za utekelezaji wa mradi huo, Injinia Wen Hongyuan kutoka China Railway, alisema kuwa mradi huo kwa sasa upo katika asilimia 5 ya utekelezaji ambapo tayari kazi ya kusafisha eneo la ujenzi na ofisi za wajenzi zimekamilika. 

Alisema ujenzi huo utahusisha matenki 6 kwa ajili kuhifadhia mafuta aina ya Diesel, matenki 5 ya kuhifadhia Petroli na matenki matatu kwa ajili ya kuhifadhia mafuta ya kuendeshea ndege.

3