WATU watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na tembo waliovamia mashamba na makazi ya watu katika vijiji mbalimbali wilayani Liwale, mkoani Lindi katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu.
Imeelezwa kuwa wanyamapori hao, katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Oktoba mwaka huu, wamefanya uharibifu wa hekta 14,000 za mazao mbalimbali, yakiwamo ya chakula na biashara ya zaidi ya wananchi 4,000 katika wilaya hiyo ya Liwale.
Ofisa Maliasili na Mazingira Wilaya ya Liwale, Deogratias Simwanza, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliotembelea wilaya hiyo kuangalia utekelezaji Mradi wa Kupunguza Migongano ya Binadamu na Wanyamapori unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani.
Simwanza alisema vifo hivyo vilitokea kutokana na kuwapo changamoto ya mgongano kati ya binadamu na wanyamapori na kusababisha wanyama hao wakali kuleta madhara na kugharimu maisha ya binadamu.
Alisema pamoja na kuwapo madhara hayo kwa binadamu, upo utaratibu wa kutoa fidia na kifuta machozi ingawa hauwezi kufananishwa na thamani ya binadamu. Wizara ya Maliasili na Utalii hutoa malipo baada ya tathmini inayofanywa na wilaya.
Alisema kuwapo migongano ya binadamu na wanyamapori wilayani Liwale kunachangiwa na eneo kubwa ya wilaya hiyo kuwa hifadhi na maeneo hayo yamehifadhiwa vizuri, hivyo kuwapo ongezeko la wanyamapori, hata wanafika katika makazi na mashamba ya wananchi.
"Tumekuwa na ongezeko kubwa la wanyamapori kwa sababu takribani vijiji vyote vimezungukwa na hifadhi, inachangia kuwapo migongano baina ya binadamu na wanyamapori na kutusababishia madhara, vikiwamo vifo," alisema Simwanza.
Mratibu wa Mradi wa Utatuzi wa Migongano ya Binadamu na Wanyamapori kutoka GIZ Wilaya ya Liwale, Debolah Missana, alisema mradi huo unakusudia kupunguza tatizo hilo na tayari umeanza kufanya kazi katika vijiji 11 na umepata mafanikio ya kuanza kudhibiti tembo kuingia katika mashamba ya wakulima pamoja na makazi ya watu.
Alisema moja ya hatua zilizochukuliwa kutatua changamoto hiyo ni kuwapa mafunzo wahifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), hata kufundishwa kuendesha ndege nyuki kwa ajili ya kufukuza tembo kidigitali.
Alisema njia nyingine ambayo hivi sasa wanaanza kuitekeleza kufukuza tembo mashambani ni kutumia mizinga ya nyuki na tayari GIZ wameshatoa mizinga 100 kwa wilaya ya Liwale na wanatarajia kuongeza mingine 200.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Goodluck Mlinga, alithibitisha vifo hivyo, akisema tembo hao kusababisha madhara kunatokana na eneo kubwa la wilaya hiyo kuzungukwa na hifadhi, zikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Pori la Akiba Selous, hifadhi za vijiji na jumuiya za hifadhi pamoja na maeneo ya uvunaji miti ya mbao.
Alisema kuwa kutokana na uhifadhi mzuri, wanyamapori wameongezeka kwa kasi, vijiji 64 vina changamoto kubwa ya kuvamiwa na makundi ya tembo (ndovu).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED