Hospitali ya rufani yajengwa kisiwani Nansio

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 03:54 PM Jan 13 2025
Hospitali ya rufani yajengwa kisiwani Nansio.
Picha: Mtandao
Hospitali ya rufani yajengwa kisiwani Nansio.

SERIKALI imeanza ujenzi wa hospitali ya rufani katika Kisiwa cha Nansio Wilaya ya Ukerewe kwa lengo la kuwaondolea adha wananchi kuvuka Ziwa Victoria kufuata matibabu ya kibingwa jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa kukagua utekelezaji wa mradi huo katika Kijiji cha Bukindo, Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Chagu Ng’oma alimtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati na ubora.

Chagu, alimtaka mkandarasi huyo, M/S Dimetoclasa Real Hope Limited kuhakikisha mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh. bilioni 25 unatekelezwa kulingana na thamani ya fedha hizo. 

Alisema serikali imetenga fedha ili wananchi wa kisiwa hicho waweze kupata huduma za kibingwa jirani na maeneo yao badala kusafiri kwenda jijini Mwanza ambako ni mbali zaidi na kwa kutumia usafiri wa maji. 

Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk. Jesca Lebba alitoa wito kwa mkandarasi huyo na mshauri elekezi kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwasilisha taarifa kila wapatapo changamoto ili kutatua  kwa pamoja na kufikia lengo la serikali la kuwapatia wananchi huduma bora za afya na za kibingwa. 

Wakala wa Usimamizi wa Ujenzi huo, Mhandisi John Bhoke aliahidi kujenga hospitali hiyo kwa kasi na kukabidhi kwa wakati kukidhi matakwa ya mkataba. 

Mkandarasi huyo alikabidhiwa mradi huo Desemba 27, mwaka jana na kuahidi kukamilisha Juni 30, mwakani. 

Serikali imetoa Sh.bilioni sita kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo.