BAKWATA yataka kushughulikiwa vihatarishi dira 2025

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:50 PM Jan 13 2025
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Mohamed Khamis.
Picha: Mauld Mmbaga
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Mohamed Khamis.

NAIBU Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikh Mohamed Khamis, ametoa wito kwa Tume ya Mipango inayosimamia uandishi wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050, kuhakikisha kuwa inazingatia na kufanyia tathmini changamoto zote zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Dira 2025 ili kuhakikisha changamoto hizo hazijitokezi tena 2050.

Sheikh Khamis ametoa kauli hiyo leo mkoani Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Umoja wa Taasisi za dini nchini Tanzania, wanaokutana kupitia rasimu ya kwanza ya Dira 2050, ikiwa ni kundi la mwisho kufikiwa na Tume ya Mipango kwaajili ya mapitio ya rasimu hiyo.

Sheikh Khamis ametolea mfano changamoto zilizojitokeza kwenye Dira 2025 kuwa ni pamoja na kutofungamana kwa sera mbalimbali ikiwemo sera ya vyama vya siasa na dira 2025 suala ambalo limesababisha kukosekana kwa vipaumbele vikuu vya Taifa kutokana na tofauti iliyopo kati ya sera, Ilani za vyama vya siasa na Dira 2025.

"Tume izingatie vihatarishi vya Dira 2025 ili kuvitengenezea mkakati maalum wa kuvidhibiti ili visikwamishe utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050," amesema.