WAKAZI wa kijiji cha Mayamaya, wilayani Bahi, mkoani Dodoma, wamepinga kumegwa eneo la shule lenye ukubwa wa ekari 27 na kupewa mtu anayetajwa kuwa mwekezaji kama fidia ya kuwajengea shule ya sekondari.
Kutokana na uamuzi huo, mvutano mkali kwa pande tatu kati ya serikali, mwekezaji na wananchi umeibuka baada ya kutolewa kwa ekari hizo 27 za Shule ya Msingi Mayamaya kama fidia ya kujengewa shule ya sekondari ya kijiji hicho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema ardhi hiyo ilitolewa kinyemela na kwamba si makubaliano, wakitaka vyombo vya dola kuingilia kati kuchunguza sakata hilo.
Mwishoni mwa wiki, wananchi walijikusanya na kwenda kung'oa alama za mipaka (bikoni) zinazotenga eneo la shule na linalochukuliwa na mwekezaji ambaye anadaiwa kupitisha katapila na kuharibu mazao waliyokuwa wamelima wanafunzi wa shule hiyo.
Shule ya Msingi Mayamaya iliyoko jirani na makazi ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango ni miongoni mwa shule chache zenye maeneo makubwa ambayo inakadiriwa kuwa na eneo la ekari 55 walizokuwa wanazitumia katika miradi ya kilimo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Irene Mwenda, alisema hakuna taarifa za kuchukuliwa eneo hilo, hata anashangazwa kuona mwekezaji kuingiza trekta kuharibu karanga na mazao mengine yaliyopandwa na wanafunzi kwa madai wameingia eneo lake.
Irene alisema shule haina taarifa za kuchukuliwa kwa eneo hilo na kwamba wasingezuia ujenzi wa sekondari hiyo.
Alisema eneo hilo alilochukua mwekezaji huyo ni upande wa barabarani ambako naye anadaiwa kutaka kujenga shule yake binafsi.
"Hivi wapi mliona watu wanafanya mambo kama tuliyofanyiwa sisi watu wa Mayamaya? Wanakaa watu wachache wanakubaliana kuuza eneo la taasisi kwa kisingizo cha kujenga shule ya sekondari wakati kwenye kata hii tunayo shule na hata madarasa hayajai.
"Kibaya zaidi walifanya figisu wakamhamisha aliyekuwa mwalimu mkuu wa hapa ambaye alikuwa anazuia ndipo wakafanikisha lengo lao," alidai Irene.
Akizungumzia ujenzi wa shule ya sekondari, mwenyekiti huyo alisema kuwa tangu mwanzo, wananchi walishirikishwa na kutoa nguvu zao katika uchimbaji msingi na kusogeza mchana ndipo wakaambiwa kuna mfadhili amejitolea kujenga shule hiyo.
"Lakini bila kushirikishwa kwenye mikutano ya hadhara na hakukuwa na maelezo kwamba mjenzi anachukua eneo la shule kama sehemu ya gharama zake," alisema.
Alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia mvutano huo, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Janeth Mayanja, aliomba mwandishi kutafuta ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Bahi kwa kuwa yeye hakuwa na taarifa za kina kuhusu mgogoro huo.
Baada ya kutafutwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bahi, Zainabu Mlawa alikiri kuufahamu mgogoro huo lakini akasema mwekezaji huyo alipewa kihalali eneo hilo la shule kwenye mkutano wa hadhara ili awajengee wananchi shule ya sekondari na baadaye kuikabidhi kwa serikali, jambo alilosema linaendelea kutekelezwa hadi sasa.
Hata hivyo, kauli hiyo ya mkurugenzi inakinzana na uamuzi uliowahi kutolewa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe (sasa Mkuu wa Wilaya ya Singida) ambaye aliwahi kusimamisha ujenzi wa sekondari hiyo kwa maelezo kwamba ulikuwa umekiuka taratibu.
Alipoulizwa na mwandishi kuhusu taratibu za utoaji maeneo ya umma, ikiwamo shule -- kwamba zinatakiwa kupitia njia zipi, Mkurugenzi Zaibanu alisema anafuatilia kama kulikuwa na ukiukwaji.
Hata hivyo, alisema hadi wakati huu anachotambua ni mwendelezo wa ujenzi wa shule ya sekondari kama fidia ya mhusika ambaye hakumtaja jina lake, ili alichukukue eneo la shule ambalo walikubaliana na uongozi wa kijiji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED