Biteko apata mwarobaini katikati ya umeme nchini

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:03 AM Jan 13 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema wizara hiyo kwa sasa inafanya maboresho makubwa katika njia zote za umeme za zamani, ikiamini ndiyo mwarobaini wa kumaliza kabisa tatizo la kukatika kwa umeme nchini.

Dk. Biteko alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipozungumza na TBC kuelekea Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini Januari 27 na 28 mwaka huu.

Alisema kuwa kwa sasa njia zote za umeme nchi nzima zimezidiwa kutokana na maendeleo ya kiuchumi na hivyo kuwa na mahitaji makubwa ya nishati hiyo.

"Ambacho ninaweza kusema ni kwamba, njia zote za umeme nchi nzima zimezidiwa, na hii ni baada ya nchi yetu kuendelea sana kiuchumi na ukitaka kupima tunaendelea kiuchumi, angalia mahitaji ya nishati hasa kwenye matumizi.

"Ninazungumzia kipindi ambacho ni karibu mwaka mmoja peke yake, mahitaji ya juu yalikuwa ni MW 1,410, leo tunazungumzia mahitaji ya juu MW 1,888. Katika historia ya nchi yetu yote, hakuna kipindi ambacho tumekuwa na ongezeko la MW 400 kwa mwaka.

"Yaani nikizungumza MW 400, maana yake unazungumza mradi mzima wa Mtera, chukua na mradi wa Kidatu na mradi mzima wa Hare, yote hiyo ni mahitaji ya mwaka mmoja. Sasa kukatikakatika huko ni lazima kutokee kwa sababu ili tufanye marekebisho ni lazima tuzime umeme," alisema.

Dk. Biteko aliwataka Watanzania wawe na subira katika kipindi hiki ambacho serikali inafanya maboresho hayo makubwa.

"Kwa mfano tunapojenga laini ya kilomita 30 na unahitaji vilevile kubadilisha transfoma, uichaji, uifanyie majaribio na vitu vyote hivyo vya kitaalamu, hiyo ni lazima itokekee, ambacho ninaweza kuwaomba watanzania ni kwamba tuwe na subira kwa sababu wakati wa mgawo tusingeweza kufanya marekebisho yoyote.

"Watuvumilie kwa sababu ni miundombinu ambayo ni mikubwa, inahitaji muda kuijenga, inahitaji fedha nyingi na uzuri ni kwamba serikali imetoa fedha, sisi kazi yetu ni kwamba kila mahali ambapo tunataka watu wapate umeme, waupate," alisema 

Dk. Biteko alisema kwa sasa taifa lina umeme wa kutosha na ziada na uzalishaji umepanda kutoka MW 1,470 hadi MW 3,077.

Alisema mpaka sasa katika Bwawa la Nyerere mitambo sita imeshawashwa na mingine mitatu inatarajiwa kuwashwa ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo na kukamilisha yote tisa.

"Hali ya upatikanaji umeme kwa kiasi kikubwa ni wa maji ambayo ni zaidi ya asilimia 56, unafuatiwa na umeme wa gesi ambao tuna MW 1,700, kwa ufupi tumepiga hatua nzuri," alisema.

Alisema kwa sasa wanachofanya ni kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme kwa watu kwa kufanyia maboresho makubwa njia zote za umeme za zamani.

"Tumeanza kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa watu, kuwafikia, kwa mfano njia tulizonazo za kusafirisha umeme, nyingi ni za zamani sana, zimezidiwa na mahitaji ya watu yamekuwa makubwa sana.

“Tunabadilisha laini, tunatoa nguzo, tunaweka nyaya mpya na transfoma kubwa, vituo vya kupozea umeme na vyenyewe tunavipanua zaidi, kituo cha Gongolamboto, Mbagala, Dege na Kipawa ambako kwa kweli tukifanya marekebisho ya vituo hivyo upatikanaji umeme katika nchi hii na kukatikakatika vitaisha kabisa," alisisitiza Dk. Biteko.