CCT yasisitiza diplomasia jumuishi kichocheo dira 2050

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:13 PM Jan 13 2025
Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa CCT, Azgard Stephen.
Picha: Mauld Mmbaga
Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa CCT, Azgard Stephen.

JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imependekeza kuwa kuelekea miaka 25 ni muhimu taifa kuimarisha nafasi ya diplomasia kama kichocheo cha maendeleo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kamati ya dili mbalimbali, Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Utetezi wa CCT, Azgard Stephen, amesema ni muhimu pia kukatolewa kipaumbele katika masuala ya sayansi, teknolojia, na diplomasia katika mapinduzi ya kiuchumi na kijamii.

“Sisi CCT tuliangalia suala la sayansi na teknolojia kwa kuzingatia jinsi dunia ilivyobadilika na mapinduzi yanayotokea. Tunapendekeza diplomasia iwe sehemu ya vichocheo vya maendeleo ili kuwezesha Tanzania kujihusisha vyema katika biashara za kimataifa na kujitengenezea nafasi bora kikanda na kimataifa,” amesema Azgard.

Azgard ameongeza kuwa mapinduzi ya kidijiti ni mojawapo ya vichocheo muhimu vya maendeleo vilivyotajwa katika rasimu ya dira hiyo, akibainisha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia na sayansi ili kufanikisha malengo ya Taifa.

1

“Mpango wetu umetaja umuhimu wa sayansi na teknolojia kama kichocheo cha maendeleo. Hata hivyo, tunashauri diplomasia nayo izingatiwe kama kichocheo, hasa katika nguzo ya uchumi ambayo inazungumzia ushiriki wa Tanzania katika jumuiya za kikanda na kimataifa,” amesema.

Pia ametoa wito wa kujumuisha diplomasia kama nyenzo ya kufanikisha maendeleo, akisisitiza kuwa diplomasia thabiti itaiwezesha Tanzania kushirikiana vyema na nchi nyingine na kujijengea nafasi imara katika biashara za kimataifa.

“Diplomasia ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha kwamba tunaweza kufanikisha mabadiliko na maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia,” amesema.

2