Tume maboresho ya kodi yaanza safari mikoani kukusanya maoni

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 04:31 PM Jan 13 2025
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue.

Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue, ameongoza wajumbe wa tume hiyo katika zoezi la kukusanya maoni ya wadau wa kodi, likianza rasmi mkoani Mwanza.

Akiendesha kikao hicho leo, Januari 13, 2024, Balozi Sefue amesema lengo la tume ni kuhakikisha mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa walipakodi na unaleta tija kwa taifa.

“Tanzania, tija yetu ya kukusanya mapato bado ni ndogo, kati ya asilimia 12 hadi 13. Hali hii haipaswi kuendelea. Angalau tunapaswa kufikia asilimia 16 ili kuweza kugharamia mahitaji muhimu ya wananchi kama ujenzi wa shule, miundombinu ya afya, na huduma nyingine za kijamii. Je, tutafikaje huko bila kuwa na mapato ya kutosha?” amehoji Balozi Sefue.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha serikali kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kujitegemea.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Mwanza (TCCIA), Gabriel Chacha, anetoa mapendekezo kwa serikali kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi. Amesema baadhi ya changamoto kubwa ni pamoja na mfumo usio rafiki wa ukokotoaji wa kodi, ambao hauzingatii hali halisi ya biashara.

1

“Tunaiomba serikali iondoe mfumo wa ukokotoaji wa kodi unaoumiza biashara na badala yake kuwepo na utaratibu wa kulipia kodi chini ya mwavuli mmoja ili kurahisisha michakato,” amesema Chacha.

Ameongeza kuwa sheria na faini zinazohusiana na kodi zinapaswa kufanyiwa marekebisho, kwani viwango vya adhabu vilivyopo sasa vinawaathiri moja kwa moja wajasiriamali wadogo.

Wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Balozi Maimuna Tarishi, na wajumbe wengine ambao ni Balozi Mwanaidi Maajar, Profesa Mussa Assad, Profesa Florens Luoga, CPA David Tarimo, CPA Leonard Mususa, CPA Rished Bade, na CPA Abubakari Abubakar.

Tume hiyo iliundwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kupokea maoni ya wadau wa kodi ili kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato nchini kwa njia shirikishi na isiyokuwa na malalamiko.

Kupitia maoni yanayokusanywa, serikali inalenga kuboresha mazingira ya ulipaji kodi, kukuza uchumi, na kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa kiwango bora zaidi.

4