Mwinyi atoa angalizo wanasiasa, viongozi dini mwaka wa uchaguzi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 09:45 AM Jan 13 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi akiwapungia mkono wananchi waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uwanja wa Gombani, Pemba jana. Kushoto ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi akiwapungia mkono wananchi waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uwanja wa Gombani, Pemba jana. Kushoto ni Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa amani na utulivu kwa kuwa tume zote mbili za uchaguzi zimeanza maandalizi ili uchaguzi huo ufanyike kwa misingi ya amani na sheria.

Vilevile, Dk. Mwinyi amesema kuwa ili kufanikisha uchaguzi huo, ni vyema viongozi wa kisiasa, dini na wananchi kudumisha amani ili kuzidi kupiga hatua za maendeleo kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Alisema hayo jana wakati akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

Rais Dk. Mwinyi alisema: "Leo (jana) ni siku muhimu ambapo miaka 61 iliyopita ukurasa mpya ulifunguliwa baada ya viongozi kujitoa mhanga na kufanya mapinduzi.

Alisema siku hiyo ni kumbukumbu ya wananchi wa Zanzibar kujikomboa  kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na madhila yaliyotokana na kutawaliwa.

Alisema kuna wajibu wa kuwakumbuka waasisi wa mapinduzi, akiwamo Hayati Abeid Amani Karume ili kunufaika na hekima na busara zao.

Rais Dk. Mwinyi alisema katika kuadhimisha miaka 61 ya mapinduzi hayo, anajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kufikia malengo, ikiwamo kudumisha amani na umoja huku watu wanaishi katika misingi ya usawa na wananufaika na rasilimali na fursa zote zilizopo bila ya upendeleo.

Alisema serikali imetafsiri dhamira ya mapinduzi kwa kuleta mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Rais Dk. Mwinyi alisema nchi imepata mafanikio makubwa katika kukuza uchumi kwa kuongeza ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi yake.

Alisema mafanikio makubwa yamepatikana katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, kuimarisha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, bandari, ujenzi wa nyumba za makazi na biashara, uimarishaji miundombinu ya michezo, huduma za afya, umeme, maji, elimu, demokrasia na utawala bora.

Rais alisema ni wajibu kuendelea na umoja na mshikamano kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, umahiri na uzalendo ili kuleta maslahi ya nchi kama walivyofanya waasisi wa mapinduzi.

Akitoa salamu za serikali katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe hizo ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alisema shughuli hiyo ni kubwa kwa maslahi ya Zanzibar na taifa na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza sherehe hizo.

Alimpongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuletea mafanikio makubwa nchi na kuyatunza na kuyalinda mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema shamrashara za miaka 61 ya mapinduzi zilianza Desemba 15 mwaka jana, miradi mbalimbali ya maendeleo ikizinduliwa na mingine kuwekwa mawe ya msingi. Miradi 113 imezinduliwa au kuwekwa mawe ya msingi katika kipindi hicho.

Sherehe hizo za Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar zilifana kisiwani Pemba, maelfu ya wananchi wakifurika kwenye Viwanja vya Gombani.

HALI UWANJANI

Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali za ngoma za asili na gwaride la askari wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na maonesho maalumu ya kijeshi.

Saa 8:45 alasiri, Rais Dk. Mwinyi aliwasili uwanjani na kupokewa kwa shangwe na nderemo. Kabla ya kuwasili kwake, alitanguliwa na Rais Samia aliyeingia uwanjani huko saa 8:00 alasiri.

Baada ya Rais Dk. Mwinyi kuwasili uwanjani, mizinga 21 ilipigwa na kukagua gwaride na kupokea maandamano ya wananchi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwamo marais wastaafu wa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi hao ni pamoja na Marais wastaafu, Dk. Amani Abeid Karume, Dk. Ali Muhamed Shein, Makamu wa Rais Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais, Abdulah, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, Makamu wa pili wa Rais mstaafu, Balozi Seif Ali Iddi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

Wengine ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Askon, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuberi Ali Maulid, Mume wa Rais Samia, Hafidh Ameir, wake wa viongozi na viongozi wa vyama vya siasa.