MASHAURI 51 yaliyofunguliwa na waliokuwa wagombea wa nafasi za uenyekiti wa mitaa, vijiji na vitongoji kupitia Chama cha ACT Wazalendo kupinga mwenendo mzima wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka jana, yanatarajiwa kutajwa leo katika mahakama mbalimbali nchini.
Kesi hizo zilizofunguliwa katika mahakama za wilaya mbalimbali za Tanzania Bara, zimeanza katika hatua ya awali ya kutolewa wito wa mahakama kuwaita wahusika (wajibu mashauri) kwa ajili ya kutajwa na kujibu mashauri.
Wilaya zilikofunguliwa kesi hizo ni pamoja na Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma, Tunduru, Tandahimba, Kilwa na Kibiti.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban, aliyotoa jana, leo Januari 13, kesi tatu tofauti zitatajwa katika Mahakama ya Mkuranga, mkoani Pwani chini ya Hakimu Kenedy Mroso.
Katika mashauri yatakayotajwa Mkuranga, mlalamikaji wa kwanza ni Mmembu Said aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Tambani, akiwashtaki Msimamizi wa Uchaguzi wa Kijiji hicho na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Juma Kizigo aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika kitongoji cha Mkoga kupitia ACT Wazalendo, anawashitaki Msimamizi wa Uchaguzi wa Kijiji cha Mkoga na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kesi ya tatu itakayotajwa kwa Hakimu Mroso, mlalamikaji ni Bakari Mchonjo anayewashtaki Msimamizi wa Uchaguzi Kitongoji cha Mikengeni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Wakili Omari Said Shaaban, ambaye pia ni Waziri wa Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema hatua ya kufungua mashauri hayo ni mwendelezo wa dhamira ya Chama cha ACT Wazalendo kupigania demokrasia na haki za wananchi alizodai ziliporwa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Imani yetu kuwa kilichotokea kabla na siku ya tarehe 27 Novemba 2024 hakikuwa uchaguzi bali uchafuzi na ahadi ya viongozi wetu ya kusimamia haki na demokrasia katika kila hatua ndiyo hii.
"Katika hatua ya sasa tunatoa wito kwa wanachama na wapenzi wote wa demokrasia nchini kujitokeza kwa wingi wakati wa kesi hizi zinapoitwa mahakamani na chama kitaendelea kutoa taarifa ya kila hatua katika mwenendo wa mashauri haya," alisema Wakili Shaaban.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED