DC Gondwe awapigia magoti wakazi wa Msikii,Munkhola kuhama hifadhini

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 03:40 PM Jan 13 2025
MKUU wa Wilaya ya Singida mkoani hapa, Godwin Gondwe amewapigia magoti wakazi wa vijiji vya Msikii na Munkhola kuwaomba waondoke ndani ya Hifadhi ya Msitu.
Picha:Mpigapicha Wetu
MKUU wa Wilaya ya Singida mkoani hapa, Godwin Gondwe amewapigia magoti wakazi wa vijiji vya Msikii na Munkhola kuwaomba waondoke ndani ya Hifadhi ya Msitu.

MKUU wa Wilaya ya Singida mkoani hapa, Godwin Gondwe amewapigia magoti wakazi wa vijiji vya Msikii na Munkhola kuwaomba waondoke ndani ya Hifadhi ya Msitu baada ya kudaiwa kuvamia kwa kilimo na ujenzi wa makazi.

Imebainika  kuwa eneo hilo la Munkhola limeanza kupata mmomonyoko wa ardhi unaoweza kusababisha madhara kama yaliyotokea Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara. 

Wakazi wa Kijiji cha Msikii na Munkhola wanadaiwa kuvamia eneo hilo na kujimilikisha kinyume na sheria na kufanya shughuli zao. 

Shughuli hizo za kilimo na ujeni wa makazi, zimesababisha mmomonyoko wa ardhi katika kijiji cha Munkhola na kuharibu nyumba zaidi ya 150 kutokana na chemchem inayotoka katika hifadhi hiyo ya Munkhola. 

Gondwe, baada ya kushuhudia uharibu huo, akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya kwenda kushughulikia mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Msikii na Munkhola baada ya kufukuta kwa muda mrefu., alipiga magoti kama msisitizo wa kuwasihi wakati hao kuondoa katika hifadhi hiyo. 

Akizungumza na wakazi wa vijiji hivyo baada ya kutembelea msitu wa hifadhi hiyo na kujionea uharibifu mkubwa kutokana na shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi,alitoa miezi mitatu kwa wanaojihusisha na shughuli hizo  kuondoka ndani ya miezi mitatu. 

Katika kuweka msisitizo wa agizo hilo, Gondwe alipiga magoti kuwaomba wakazi hao kuhama ndani ya msitu huo hatua ambayo iliwashangaza wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara. 

"Nisikilize hatutanii, napiga magoti miezi mingapi... mitatu, tokeni kwenye hifadhi,niruhusuni nisimame Mwenyekiti wa Kijiji amenielewa," alisema Gondwe huku wananchi wakipigwa butwaa kwa kiongozi kama yeye kuwapigia magoti. 

Alisema kutokana na uharibifu unaofanyika ndani ya msitu huo kuna maporomoko yanapeleka maji ndani ya kijiji cha Munkhola na kusababisha vyoo kutitia huku nyumba zikijaa maji na hivyo kuhatarisha maisha ya watu. 

Gondwe, aliwataka wakazi hao kutambua kuwa wana wajibu wa kutunza hifadhi kwa manufaa ya vizazi vyao na kwamba kuharibu hifadhi ni ubinafsi na kukosa mvua, lakini pia kunahatarisha kutokea maafa kama yaliyotokea wilayani Hanang' mkoani Manyara.

 "Usiwe chanzo cha kuharibu hifadhi, maelekezo ni kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Singida kupitia idara ya ardhi nitahesabu siku 14 kuanzia jana (Jumatatu) wataalam wawe wamefika na kuonesha mipaka ya vijiji hivyo,” alisisitiza. 

Alisema wananchi walioziwa ardhi wametapeliwa kwa sababu wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni mkutano mkuu wa kijiji na wajumbe ni wananchi na sio Halmashauri Kuu ya Kijiji. 

"Kama uliuziwa ardhi na Halmashauri ya Kijiji na kijiji kinasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya wamekutapeli kachukue hela yako, ardhi ya kijiji sio mali ya Halmashauri ya Kijiji, " alisema Gondwe. 

Kwa upande wao, wakazi hao, walisema hali ni mbaya katika vijiji vyao kutoka na maji kujaa maji na vyoo kutitia kutokana na uharibifu wa msitu huo.