BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limesisitiza kuhusu udhibiti wa michezo ya kubahatisha na kamari kwa vijana kuelekea 2050, ikisema michezo hiyo imekuwa na athari nyingi ikiwemo kufifisha nguvu kazi ya jamii na kuwatia vijana kwenye umaskini.
Hayo yameelezwa leo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kamati ya dini mbalimbali, kuhusu rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akitoa mapendekezo kwa niaba ya BAKWATA, Naibu Katibu Mkuu Sheikh Mohamed Khamis, pia ameshauri serikali kuhakikisha kuwa mipango ya kitaifa inasimamiwa na kushughulikiwa na wizara moja inayojitegemea badala ya kuhamisha idara hiyo kila wakati kwenye wizara mbalimbali ndani ya serikali.
"Pia kuelekea 2050 ni muhimu kama Taifa kuwa na huduma za kifedha jumuishi na ambazo zitazingatia sheria za kiislamu ili kutengeneza usawa bila ya ubaguzi wa kidini," amesema.
Pia amesisitiza umuhimu wa kutilia mkazo kilimo cha mageuzi na kibiashara kuanzia ngazi ya familia ili kuhakikisha kuwa kinakuwa na tija kiuchumi na kuwa sehemu ya kuwaondoa watanzania kwenye wimbi kubwa la umaskini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED