BAKWATA wataka maslahi ya walimu kuboreshwa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:25 PM Jan 13 2025
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikhe Mohamed Khamis.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Sheikhe Mohamed Khamis.

BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wametoa wito kwa serikali kupunguza gharama za matibabu pamoja na kuboresha maslahi ya waalimu ili kuendelea kukuza nguvu za kiuchumi na kujenga jamii iliyoelimika kuelekea miaka 25 ijayo.

Hayo yalipendekezwa leo mkoani Da es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa BAKWATA Sheikh Mohamed Khamis, wakati wa mkutano wa kamati ya dini mbalimbali kuhusu rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Pia amehimiza umuhimu wa serikali kusimamia ratiba na mapumziko kwa wanafunzi wa shule za serikali na binafsi kama sehemu ya kuhakikisha kuwa kunakuwa na ulinganifu wa masomo na mapumziko kwa wanafunzi, ili wapate muda wa kushiriki shughuli zingine.

"Pia tunaishauri serikali kutenga viti vya uwakilishi wa taasisi za kidini kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ulivyo uwakilishi mwingine kwenye chombo hicho muhimu cha kutunga sheria," amesema.

Aidha Bakwata wamehimiza umuhimu wa kutunza mazingira kuelekea mwaka 2050, kutungwa kwa sheria nakuwekwa mkakati wa kudhibiti bidhaa bandia pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani kwa kupunguza gharama za kutembelea vivutio vya utalii sambamba na kutoa ruzuku kwa taasisi zote zinazotoa huduma kwa jamii bila ya ubaguzi.