KOCHA Mkuu wa timu ya wasichana wenye umri chini ya miaka 17 ya JKT Queens, Ester Chabruma, amesema wamejipanga vema kupata pointi tatu katika mchezo wao wa leo dhidi ya City Lights FC ukiwa ni mwendelezo wa mashindano ya CAF U-17 ya Gift Girls Integrated Football Tournament (GIFT), yanayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi, Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe jana, kuelekea mchezo huo utakaopigwa leo majira ya saa 12:00 jioni, Chabruma alisema malengo yake ni kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na kwamba wachezaji wake wote wana morali ya juu.
"Tumejipanga vema kuhakikisha tunaendeleza ushindani katika mchezo huo ambao ninaamini utakuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa," alisema Chabruma.
Alisema hana wasiwasi na mchezo huo kwani amewaandaa vizuri wachezaji wake ili wapate ushindi katika mchezo huo.
Aidha, alisema anawashukuru mashabiki kutokana na ushirikiano mkubwa wanaowaonesha pindi timu yao inapokuwa inacheza.
Mpaka sasa JKT Queens inashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi sita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED