Wananchi wa maeneo ya pembezoni ambako kulikua na changamoto ya mawasilino ya simu wameanza kunufaika baada ya serikali na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc kuwafikishia huduma karibu.
Huduma hizo zimeanza kuwawezesha kuwasiliana bila vikwazo vilivyokuwepo awali kutuma, kupokea na kutoa fedha na kutumia intaneti yenye kasi kwa ajili ya matumizi mbalimbali hatua inayoongeza matumizi ya teknolojia kidijitali.
Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Vodacom Tanzania Plc, George Venanty akizungumza na gazeti hili alisema maboresho kwenye teknolojia yaliyolenga minara ya kusambaza mawimbi imeongeza wigo wa mawasiliano kwa wananchi wengi walio pembezoni mwa makao makuu ya mkoa.
“Sambamba na mkakati wetu wa kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma zenye viwango vya juu, Vodacom tumechukua hatua kuboresha mtandao wetu. Tumefanya maboresho katika maeneo mbalimbali katika kanda yetu ikiwamo teknolojia ya minara yetu lengo likiwa kuimarisha mawasiliano ili watumiaji wanufaike na matumizi ya intaneti,” alisema Venanty.
Aliongeza kuwa wamefikia maeneo mapya na maeneo ambayo yalikua yamefikiwa kumefanyika maboresho ya kuongeza kasi yenye manufaa kwa watumiaji ili waweze kunufaika na mtandao wa kampuni hiyo.
Alitaja maeneo yaliyo nje ya miji mikubwa ya Arusha, Moshi, Babati na Tanga yaliyonufaika kuwa ni Maramba, Gomba, Mgagao, Monduli na Baray ambayo teknolojia ya mawasilino imeboreshwa kwa minara kuongezewa uwezo ili wateja wafurahie huduma za kidijitali na kasi zaidi.
Mkuu huyo wa Kanda ya Kaskazini alisema kwamba mafanikio hayo yameletwa kwa ushirikiano na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), akirejea makubaliano yaliyosainiwa mbele ya Mheshimiwa Rais mnamo mwezi Mei mwaka 2023 jijini Dodoma kupitia mpango wa kuiendeleza Tanzania kidijitali (Digital Tanzania Project).
“Tunaposema Vodacom inaongoza kwa mtandao wenye kasi tunamaanisha ni hizi juhudi tunazozifanya mara kwa mara kwa ushirikiano na serikali yetu, ambapo tumekuwa tukiangalia mahitaji ya watumiaji ambao ni wateja wetu, hatua hii imesaidia kuwapa huduma bora watumiaji ambao walikuwa maeneo ambayo watumiaji ni wengi ukilinganisha na uwezo,” alisema Venanty.
Venanty alisema maeneo ambayo hayakua na huduma za mawasiliano kabisa wameshirikiana na serikali kuyafikia ili kila anayetaka kuwasiliana anafanya hivo bila vikwazo akitaja baadhi ya maeno hayo ni Gerai, Kimokouwa, Burka, Songoro, Olmot, Terrat, Enduimet, Kirua Vunjo, Leguruki, Maweni, Mabogini na Esiralei.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Kanda ya Kaskazini alisema watumiaji wa Vodacom kupitia kampeni inayoendelea ya ‘Ni Balaa! Kila mtu ni mshindi’ wameendelea kunufaika na zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu zinazotolewa kila wiki na kila mwezi, ambapo pia washindi wakuu katika kampeni hiyo watapendekeza shule ambazo kampuni hiyo itatoa misaada kwenye maktaba ili kuboresha elimu katika maeneo zilipo shule hizo. Mpaka sasa washindi wakuu wanne wamebahatika, huku mmoja anayetokea jijini Arusha akiondoka na kitita cha shilingi milioni 20 huku akichagua shule ya msingi Muriet kama mnufaika wa maboresho ya maktaba.
Aliwataka wateja wa kampuni hiyo kuendelea kutumia bidhaa na huduma ili waendelee kufurahia na kujishindia zawadi zenye thamani mbalimbali hadi fedha taslimu kiasi cha Sh.20 milioni.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED