RC akemea biashara usafirishaji binadamu

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 12:51 PM Sep 13 2024
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego
Picha:Mtandao
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amekemea usafirishaji haramu wa binadamu hususani wenye ulemavu ambao wanakwenda kutumikishwa kama mitaji ya kuombea fedha.

Alikemea hayo juzi wakati akifungua Kongamano la Wanawake Kanda ya Afrika Mashariki na Kati wa Kanisa la Waadventista Wasabato linalofanyika eneo la Ititi, Manispaa ya Singida na kushirikisha zaidi ya wanawake 2,000 kutoka nchi 11.

"Niwaombe wanawake tusimame imara kulikemea hili kwani tukijisahau linaweza kushamiri na kujikuta katika jamii zetu tunasababishiana ulemavu wa makusudi," alisema.

Dendego aliwakumbusha wanawake kutimiza kikamilifu jukumu la wazazi na walezi kwa kusimamia vyema maadili ya watoto wa kike na wa kiume.

"Sote tumekuwa mashuhuda wa athari zinazotokana na kumomonyoka kwa maadii kunakopelekea kuibuka kwa vitendo ambavyo ni kinyume cha mila, desturi na utamaduni wa kiafrika," alisema.

Alisema kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anakemea na kupinga vitendo vya uhusiano wa jinsia moja kwa kuwa suala hili linaumiza jamii, linapoteza nguvu kazi ya taifa na ni haramu katika imani ya dini zote na dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Dendego alilipongeza Kanisa la Waadventista Wasabato kwa kujenga kituo ambacho kitakuwa kinasaidia kutoa mafunzo ya stadi za kazi waraibu wa dawa za kulevya, watoto wa mitaa na makahaba ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Kituo hicho ambacho ujenzi wake unaendelea, kinajengwa na kanisa hilo kupitia dara ya wanawake kwa fedha zinazochangwa na wanawake kutoka nchi 11.

"Binafsi ninawapongeza sana kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa mwanamke katika jamii kwa kuwapa fursa ya kumtumikia Mungu na kuzisaidia jamii zetu," alisema.

Alisema ni ukweli mtu kuwa Mungu amewapa wanawake uwezo mkubwa na iwapo watatumia fursa kikamilifu familia, jamii, taifa na mataifa yatastawi kutokana na uwezo na vipawa vya kipekee ambavyo Mungu amewapa wanawake.

"Hapa kwetu Tanzania kuna usemi usemao wanawake wakiwezeshwa wanaweza, ninataka wanawake wenzangu tutoke kwenye kifungo cha usemi huu hatuhitaji kuwezeshwa bali tunapaswa kujiamini kuzitambua fursa na kuweka jitihada zetu sisi wenyewe ili kuzitumia kwa manufaa yetu,jamii nanl taifa kwa ujumla," alisema.

Alisema kuwa wanawake ndiyo chanzo cha jamii na walezi wa watoto na wanaume hivyo hakuna mafanikio katika jamii wala kwa mwanaume bila uwepo wa mwanamke imara nyuma yake.