Askofu Haverland,Askofu Kutta kusaidia wananchi kupata maji,elimu, afya na kilimo

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 03:38 PM Sep 16 2024
Mwadhama Askofu Mkuu wa Kanisa la  Kiaskofu la Kianglikana duniani, Mark Haverland, ( wa pili kulia) akimshika mkono Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini Tanzania, Elibariki Kutta kama ishara ya kumuapisha katika Ibada ya Litrugia iliyofanyika eneo la Mlali
Picha: Grace Mwakalinga
Mwadhama Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiaskofu la Kianglikana duniani, Mark Haverland, ( wa pili kulia) akimshika mkono Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini Tanzania, Elibariki Kutta kama ishara ya kumuapisha katika Ibada ya Litrugia iliyofanyika eneo la Mlali

MWADHAMA Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiaskofu la Kianglikana duniani, Mark Haverland, ameahidi kumsaidia Askofu Mkuu wa kanisa hilo Jimbo la Tanzania, Elibariki Kutta, kwa kushirikiana na Serikali kutekeleza ahadi zote alizoahidi kwa wananchi katika sekta za maji, afya, Elimu na kilimo.

Askofu Mkuu Haverland, alitoa kauli hiyo jana Septemba 15, 2024 katika Litrujia maalum ya  kumsimika Kutta kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Jimbo la Tanzania.

Ibada hiyo hiyo ilifanyika Kijiji cha Mlali, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, ambako ni makao makuu ya kanisa hilo nchini.     

Mwadhama Haverland alisema Askofu Kutta ameonesha nia ya dhati kuwasaidia watanzania wenzake kuwapa huduma za kiroho  na maendeleo  kwa kuwaboreshea huduma za kijamii.

“Nimefurahishwa na mipango ya Askofu Kutta kutaka kuwasaidia watanzania wenzake kuwapatia huduma za kijamii nami naahidi kumsaidia kutekeleza na tutashirikiana na Serikali kufanikisha,” alisema Haverland.

Akizungumza baada ya kuapishwa na Mwdhama Haverland, Kutta alikiri imani walionayo wana-Anglican kwake na kusema ana deni kubwa kwao katika suala la maendeleo kwenye sekta za maji, afya, elimu, michezo na kilimo.

1

Viongozi wa madhehebu mbalimbali wa dini ya kikristo na viongozi wa kiislam wamempongeza Askofu Kutta kuaminiwa wa Anglikana na kusimikwa kuwa Askofu Mkuu wa kwanza Tanzania wakimsisitizia kuhubiri amani na upendo ndani ya kanisa.

Akizungumzia salamu  za  Serikali kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Askofu wa Kanisa la Marovian Tanzania na Afrika Mashariki, Emmaus Mwamakula, alisema wameahidiwa kupewa ushirikiano katika kutumiza majukumu yao.

Alimkaribisha Kutta katika utumishi  wa Kiaskofu na kumuomba kuwa mstari wa mbele kuhubiri, amani haki na kuishauri Serikali masuala  yanayolenga  kuleta  Maendeleo katika Taifa.
 

Aidha alieleza kufurahishwa na misingi ya kanisa hilo ambalo linaamini kwenye  uaskofu unaozingatia mnyororo wa kutangaza neno la Mungu.

Sheik wa Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), Kata ya Mlali, Ramadhan Ngiriye, aliomba kanisa hilo kudumisha amani, upendo na mshikamano.

Alisema uapisho wa Askofu Kutta ni hatua muhimu katika kuwaunganisha wanaumini kufuata misingi ya imani na kuwa na hofu ya Mungu.