BAADA ya kukithiri kwa matukio ya wananchi kushambuliwa na makundi ya nyuki katika maeneo mbalimbali nchini, wadau wa maendeleo wameanza kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuepuka madhara ya wadudu hao.
Shirika la Maendeleo Vijijini (RDO), ndilo limejitosa kutoa elimu kwa wananchi ambapo limewataka wananchi kujikinga kwa kuziba midomo, masikio na macho, pale wanapokutana na kundi la nyuki.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Mafinga mkoani Iringa, Ofisa Nyuki RDO, Teddy Pagi alisema binadamu aking’atwa na nyuki kwenye maeneo hayo ya wazi huwa ni rahisi kupoteza maisha.
Alisema nyuki huwa wanachagua sehemu hizo muhimu kwa binadamu kuuma na kwamba sehemu hizo zikivimba ni rahisi binadamu kupoteza maisha kwa maelezo kuwa zikivimba inamuwia vigumu binadamu kupumua.
Kutokana na hilo alisema watu wanapaswa kuwa makini na siyo kukimbia peke yake bila kuwa na tahadhari yoyote ile kwenye viungo vya mwili wake.
Mbali na madhara ya nyuki pia alizitaja baadhi ya faida zitokanazo na mazao ya nyuki ikiwamo asali na maziwa ambavyo vinatumika kama chakula na dawa pamoja na sumu ambayo hutumika kama malighafi.
Alisema asali inatumika kama tiba katika matatizo mbalimbali ambazo binadamu anakutana nazo ikiwamo kuungua moto katika baadhi ya sehemu za mwili.
Alisema sumu ya nyuki inatumika kama kinga ya kuimarisha viungo vya mwanadamu yeyote yule isipokuwa sehemu ya ulimi, pua macho na masikio.
Hivyo, aliishauri jamii kufuga nyuki kwa wingi ili wavune mazao yake ambayo yatawapa faida wao na familia zao.
Pia alitoa ushauri kwa wafugaji wa nyuki kuhahakikisha wanatumia mizinga mizuri ambayo nyuki watatengeneza asali itakayowapa manufaa.
Alisema lengo lao ni kuona jamii inafaidika na mazao ya nyuki na siyo kuwakimbia badala yake wafuge ili wapate faida kupitia mazao yanayotolewa na nyuki.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED