Wilaya 106 Tanzania Bara zaunganishwa na Mkongo wa Taifa

By Allan Isack , Nipashe
Published at 05:59 PM Sep 18 2024
Mkurugenzi wa Ufundi na Undelezaji kutoka TTCL,Mhandisi Cecil Francis.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Ufundi na Undelezaji kutoka TTCL,Mhandisi Cecil Francis.

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL),limesema kati ya wilaya 139 zilizoko Tanzania Bara,hadi sasa tayari wamefanikiwa kuunganisha wilaya 106,katika mkongo wa taifa wa mawasiliano.

Hayo yamesema leo Sempemba 18,2024, na Mkurugenzi wa Ufundi na Undelezaji kutoka TTCL,Mhandisi Cecil Francis,wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kongamano la Connect 2 Connect.

Kongamano hilo,limefunguliwa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa,na limewakutanisha wadau wa mawasiliano wa ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema kwa wilaya 33 ambazo bado hazijafikiwa na mkongo wa taifa wa mawasiliano,mwaka huu wa fedha wa 2024/2025,serikali imeshatenga bajeti ya kwenda kukamilisha shughuli hiyo,ili kuhakikisha wilaya zote zinaunganishwa na zianze kupata huduma bora.

Alisema mkongo wa mawasiliano wa taifa ni kiungo kikuu cha mawasiliano ya sauti na Intaneti ambapo inaunganishwa na mikongo ya baharini ambayo inaleta Intaneti nchini.

“Mkongo wetu wa taifa wa mawasiliano ni kiungo kikuu cha mawasiliano ya sauti,lakini vilevile na Intaneti na tunaunganisha na mikongo ya baharini ambayo inatuletea Intaneti hapa nchini na sisi pia tunaunganisha na nchi za jirani za Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi,Zambia na Malawi.

“Tunamaunganisho yamekwenda mpaka Msumbiji na tumeanza kuingia maunganisho yatakayofanya tuingie hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),kupitia Ziwa Tanganyika.alisema Mkurugenzi huyo wa Ufundi”

Pia alisema shirika hilo,linaendelea kuboresha maunganisho ya mkongo kwa kusogeza kwenye vituo vya baharini vilivyoko Mombasa nchini Kenya.

“Kazi kubwa tuliyonayo TTCL,ni kuhakikisha tunatoa mchango wa mawasiliano kwa mkongo tunayojenga inafika kila sehemu ikiwa na ubora wa hali ya juu kwa ajili ya kufikisha huduma kwa wananchi na kupunguza gharama za matumizi,”alisema.

Alisema shirika hilo,kupitia mkongo wa taifa wa mawasiliano wamefanya kazi ya kuunganishwa kwa mawasiliano mikoa kwa mikoa na wilaya kwa wialaya.

“Sisi TTCL,tukiwa kama chombo cha serikali tumepewa dhamana ya kutoa huduma za mawasiliano hapa nchini,”alisema.  

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Helios towers,Gwakisa Stadi,alisema kampuni hiyo kwa hapa nchini inasimamia minara zaidi ya 400 na wana wateja zaidi ya 10000 ambao ni watumiaji wa minara hiyo.

Alisema kazi kubwa ya mirana hiyo,ni kuunganisha huduma za mawasiliano na wateja wao wakubwa ni makampuni ya simu,kampuni za usambazaji wa Inteneti na televisheni zilizoweka vifaa vyao vya mawasiliano kwenye minara hiyo.