Serikali yabeba gharama za mazishi waliouawa Dodoma

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:19 AM Sep 19 2024
Baba wa familia ambaye imepoteza watu watatu na mkewe kujeruhiwa na watu wasiojulikana usiku wa kumkia jana (Septemba 16,2024), Robert Mgema akizungumza na waandishi wa Habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Septemba 17,2024.
Picha:Mtandao
Baba wa familia ambaye imepoteza watu watatu na mkewe kujeruhiwa na watu wasiojulikana usiku wa kumkia jana (Septemba 16,2024), Robert Mgema akizungumza na waandishi wa Habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Septemba 17,2024.

SERIKALI imegharamia maziko ya miili ya watu wawili kati ya watatu waliouawa katika Kata ya Nala, jijini Dodoma.

Juzi kuliripotiwa tukio la watu watatu, watoto wawili wa familia moja na dada wa kazi, katika eneo hilo. 

Waliofariki dunia ni Milcah Robert (12), aliyehitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Chihoni, Fatuma Mohamed (20) na dada wa kazi aliyetajwa kwa jina moja la Micky (16), huku mama wa famili hiyo Lusajo Mwasonge(40) akijeruhiwa. 

Mwili wa dada wa kazi ulisafirishwa jana na ndugu zake kwenda mkoani Geita, huku miili miwili ya watoto ikizikwa mkoani Dodoma. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa familia hiyo, Gwano John, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ndiyo imegharamia baadhi ya gharama za mazishi ya watu hao. Baba wa familia hiyo ni mtumishi wa halmashauri hiyo. 

"Msiba huu ni wa kwetu wote tunatangulia kuzika wa hapa Dodoma, mmoja alizikwa jana na tutaondoka na huu mwili mwingine kuelekea Geita kwa kuwa mwili umeharibika na tumezungumza na ndugu muda wowote tutakaofika itabidi tuzike," alisema. 

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Anania Amo, alisema wanaendelea na uchunguzi wa kuwatafuta waliohusika na tukio hilo. 

Ndugu wa dada wa kazi, mkazi wa Kahama, Ramadhan Issa, alisema binti huyo ni mtoto wa kaka yake na walikumbwa na taharuki kutokana na taarifa waliyopokea kueleza kuwa amechinjwa. 

"Wazazi walipopokea taarifa za kifo, mazungumzo yaliyoongelewa wakadhani wamesusa kutokana na kukosa taarifa kamili, lakini mwisho wa siku familia ikawa na jazba. Gharama za usafirishaji wengine wakapendekeza miili yote izikwe huku (Dodoma)," alisema. 

Alisema kwa taratibu zao, mtu akifariki dunia ni lazima asafirishwe akazikwe nyumbani, kwamba walikutana na mwajiri wake na kukubaliana kuendelea na maandalizi ya kusafirisha mwili.