Mtoto wa miaka sita alivyoomba msaada watu watatu wakiuawa

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:22 AM Sep 18 2024
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo
Picha: Mtandao
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo

JESHI la Polisi mkoani Dodoma limeeleza mtoto mwenye umri wa miaka sita alivyoomba msaada katika tukio la mauaji ya watu watatu Mtaa wa Segubwawani, Kata ya Nala, jijini Dodoma.

Akizungumzia tukio hilo lililotokea juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Anania Amo alisema kuwa watu hao walikutwa wamefariki dunia huku mama anayemiliki nyumba yalimofanyika mauaji, akijeruhiwa na watu wasiojulikana.

Alisema kuwa katika tukio hilo, hakuna jirani ambaye alisikia kelele, bali mtoto aliyetumwa kwenda katika familia hiyo kufuata redio waliyoazima, alirudisha habari kuwa hakupata ushirikiano.

Kamanda Amo alisema kuwa kutokana na hali hiyo, majirani walikwenda katika nyumba hiyo na kusikia sauti ya mtoto wa miaka sita ambaye alikuwa katika nyumba hiyo akipiga kelele kuomba kufunguliwa mlango.

"Mtoto huyo hajajeruhiwa, ndiye alipiga kelele, akiomba kufunguliwa maana milango ilikuwa imefungwa. Ndipo baadaye waligundua kuwa kuna mauaji yamefanyika," alisema.

Alifafanua kuwa waliouawa ni watoto wawili wa familia moja ambao miili yao imekutwa imeungua moto huku mfanyakazi wa ndani, akikutwa na majeraha kichwani.

Kamanda Amo alisema kuwa mama alijeruhiwa, aliwahishwa hospitalini kupata matibabu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Segubwawani, Kata ya Nala, Jeremia Molima alisema alipewa taarifa ya tukio hilo juzi saa 9.45 alasiri na alipofika katika eneo hilo alikuta watu wanaingia ndani na kuwaomba watoke, wasubiri askari polisi wafike.

"Baada ya kufika, nilikuta watoto wawili wameungua kwa moto, halafu kuna dada wa kazi amelala kifudifudi amekufa, anaonekana kichwa chake kimeshambuliwa kwa sababu kwenye sakafu na damu imeganda.

"Tumemkuta mama mwenye nyumba akiwa hoi, ameshambuliwa, alikuwa akitamka kuwa anajihisi maumivu, anaomba akalale," alisema.

Alisema kuwa walichokifanya ni kumwita bodaboda kwa ajili ya kumwahisha katika Zahanati ya Nala kwa ajili ya huduma ya kwanza na wakati wakiwasiliana na askari polisi kata ambaye aliwaeleza kuwa alikuwa njiani akielekea eneo la tukio.

Molima alisema kuwa baba wa familia aliyemtambulisha kwa jina la Robert Mgema, ni mwalimu mkoani Singida, hivyo katika nyumba hiyo walikuwa wanaishi mama, watoto wake watatu na mfanyakazi wa ndani. 

"Juzi hapa walikuwa na sherehe ya mtoto aliyemaliza darasa la saba (mmoja kati ya waliouawa), hivyo baba wa familia alifika katika sherehe ya kumpongeza mtoto wao na haikufahamika wakati tukio linatokea kama alikuwa amesharejea katika kituo chake cha kazi au la.

"Inaelekea watu waliwavamia, wakawapiga hadi kuwaua, lakini hawa watoto wawili walioungua ndio tunashindwa kupata majibu ya haraka," alisema.

Kiongozi huyo alisema kuwa hakuna dalili ya moto kuwaka muda wa karibuni na hivyo wanahisi kuwa tukio hilo lilifanyika usiku.

Aliongeza kuwa Jumamosi walipokuwa na sherehe ya mtoto wao ya kumaliza darasa la saba, walikwenda kuazima redio kwa jirani kwa ajili ya sherehe.

"Leo (jana), mwenye redio alimtuma mtoto mdogo kwenda kuifuata lakini alipofika alikuta milango yote imefungwa, pamepoa na hakuna mtu anayeitika.

"Alirudi nyumbani kuwaeleza hali hiyo, ndipo majirani wakaenda. Lakini ndani ya nyumba kulikuwa na mtoto mdogo (ambaye hakuguswa), baada ya kuita kwa muda ndipo mtoto aliitika na kusema anaogopa kufungua mlango," alisema.

Alisema kuwa ndipo walipofungua wenyewe kwa nje na kuingia ndani na kukutana na mauaji hayo huku nguo zikiwa zimevurugwa, ziko chini na televisheni iko ukutani na haijaguswa kwa lolote.

Kwa mujibu wa Kamanda Amo, waliouawa ni Milcah Robert (12) aliyehitimu darasa la saba Shule ya Msingi Chihoni, Fatuma Mohamed (20) na dada wa kazi aliyetambulika kwa jina la Micky (16).

"Mama aliyejeruhiwa kwa kupigwa anaitwa Lusajo Mwasonge(40), ni mjasiriamali, alipigwa na kitu butu kichwani, anaendelea kupatiwa matibabu. Jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi wa Dodoma kama ulivyo utamaduni wao kuendelea kushirikiana na jeshi hilo ili kuhamimisha waliotekeleza uhalifu huu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani," alisema.

MMOJA ANASHIKILIWA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema jana kuwa mtu mmoja anashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusu undani wa tukio hilo.

"Tuendelee kuchukua tahadhari za kiusalama, tuwe na daftari la mkaazi, kila mtu awe na orodha ya watu wa mtaa wake na ikitokea kuna mgeni amekuja aorodheshwe na amekuja kwa shughuli ipi ili kama kuna jambo lolote la shaka litolewe taarifa," alisema.

Pia alihimiza kuwapo ulinzi shirikishi utakaohusisha vijana wenye mafunzo ili wasaidie kufanya doria.

BABA ALONGA

Baba wa familia hiyo, Mwalimu Mgema anayefanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, alisema kuwa Jumamosi alikwenda Dodoma kwa ajili ya mahafali  katika Shule ya Msingi Chihoni na siku hiyo hiyo alirejea Singida kutokana na majukumu aliyokuwa amepangiwa na siku ya Jumapili aliwasiliana kwa ujumbe mfupi na mkewe.

"Jioni niliwahi kulala kutokana na uchovu, mke wangu alinitafuta saa tatu usiku na isivyo bahati sikusikia simu, asubuhi nilipoamka nikapiga simu, lakini sikufanikiwa kumpata hadi saa nane mchana na si kawaida, nikapigiwa simu saa 10 jioni na jirani yangu Baba Kelvin.

"Akasema nyumbani kwangu hakueleweki, hajaona anayetoka nje. Nikamwuliza 'hakuna mtu yeyote?'. Akasema 'kuna mtoto ndani anaitika, tunamwambia afungue mlango, anasema anaogopa'," alisema.

Alisimuliwa kuwa baadaye alipokea simu ya jirani mwingine ambaye alimpa taarifa kuwa wamemwangalia dirishani na kuona binti wa kazi amelala chini na kuna damu, alilazimika kuanza safari kutokana na taarifa hiyo.

"Nikiwa njiani ninakuja, nikapigiwa tena kuwa polisi wameingia watu watatu wamefariki, nikauliza 'ni kina nani?' Sikupata majibu, nikaambiwa polisi wanaendelea na uchunguzi na nilipofika muda wa saa moja jioni nyumbani na kuomba nioneshwe waliofariki dunia, na kuuliza kuhusu mtoto wangu mdogo anayeitwa Caren, nikajibiwa ndiye aliyefungua mlango," alisema.

Mwalimu huyo alisema kuwa nyumbani kwake aliacha watu watano; mabinti watatu wakubwa na kati yao, mmoja amehitimu darasa la saba na binti mdogo ndiye aliyebaki hai.

"Inasikitisha sana, sijawahi kuwa na uhasama na mtu, tuna miezi sita tumehamia pale, sina mgogoro na mtu yeyote, ninalaani vikali sana, hatuwezi kwenda kwa mtindo huu, wameua watu ambao wangekuja kutusaidia, wamezima ndoto ya mwanangu, alitaka kuwa mhandisi," alisema.