Programu ya imarisha uchumi na Mama Samia IMASA yazinduliwa Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 04:18 PM Sep 18 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Picha:Marco Maduhu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.

PROGRAMU ya imarisha uchumi na Mama Samia (IMASA)imezinduliwa mkoani Shinyanga,kwa lengo la kuwezesha wananchi kiuchumi kupitia kwenye vikundi.

Programu hiyo imezinduliwa Septemba 17,2024 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.

Macha akizungumza wakati wa uzinduzi program hiyo, alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake mazuri ambayo amedhamilia kuwainua wananchi kiuchumi kupitia kwenye muunganiko wa vikundi.

Alisema suala la kuwezesha wananchi kiuchumi, linapaswa pia kutumia fursa zilizopo kwa kila mkoa, ambapo katika mkoa wa Shinyanga, kuna fursa za kilimo cha pamba, mpunga, tumbaku, dengu,choroko, ambapo wananchi wanapaswa kujiunga kwenye vikundi na kuongeza thamani mazao hayo na hata kufungua viwanda.

Amezungumzia pia fursa ya uanzishwaji viwanda vya maziwa, kwamba katika Mkoa wa Shinyanga hakuna kiwanda ambacho kina zalisha maziwa, na kwamba maziwa mengi ambayo yanauzwa kwenye “super market” mengi yanatoka mikoa mingine ikiwamo Tanga, Iringa, Mara, fursa ambayo wananchi wanaweza kujiunga kwenye vikundi na kuitumia ipasavyo na kuinuka kiuchumi. 

“Shinyanga maziwa yapo lakini hakuna kanuni za uzingatiaji wa afya, ambapo wananchi wanapaswa kuyaongezea thamani maziwa hayo kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kuuza maziwa kupitia kwenye vikundi na kuinuka kiuchumi,”alisema Macha.

Aidha, alisema program hiyo ya imarisha uchumi na Samia, kwamba katika Mkoa wa Shinyanga kuna machimbo makubwa ya madini, lakini wananchi kupitia vikundi watatumia fursa ya kutoa huduma mbalimbali kwenye migodi hiyo.

Mshauri wa Rais Samia wanawake na makundi maalumu Sophia Mjema,alisema dhamira ya Rais ya kuanzisha program hiyo amelenga kuwainua wananchi wote kiuchumi, na hakuna ambaye ataachwa na wala hakuna kuingiza vikundi kwenye kanzi data kwa urafiki na hata kujuana.

Amesema Rais Samia amewatuma pia kufufua majukwaa yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo yalikuwa yamelala, na ndiyo maana wanazunguka mikoa yote na sasa wapo kwenye mkoa wa 16 Shinyanga, ili kutambulisha program ya imarisha uchumi na mama samia, kwa kukutana na viongozi pamoja na makundi ya wanawake,vijana na watu wenye mahitaji maalum.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Taifa (NEEC) Beng’i Issa, alisema baraza hilo lilianzishwa mwaka 2004, na kwamba katika sera hiyo inaelezea hali ya ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchumi ni duni.

Alisema program hiyo inasimamiwa na Ofisi ya Rais Ikulu, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi, na itafanyika katika mikoa na wilaya za Tanzania bara na visiwani.

Alisema hatua ya kwanza ya proramu hiyo itahusisha uandaaji wa kanzi data ya walengwa,utambuzi wa shughuli za kiuchumi za wadau na mahitaji maalumu ya uwezeshaji, kwa vikundi vilivyotambuliwa au sajiliwa vya wanawake,vijana na watu wenye mahitaji maalumu.

Alisema awamu ya pili itahusisha uandaaji wa proramu maalumu za uwezeshaji kiuchumi kwa makundi yaliyorasimishwa, kulingana na mahitaji yaliyoonekana katika uchakataji wa takwimu.

“Programu hii ni ya miezi sita ambayo ilianza januari 2024 hadi julai na tumelenga kuwafikia wanufaika 62,000 na hadi sasa tumevuka lengo tumefikia wananchi zaidi ya elfu 70 na hii inaonyesha muitikio ni mkubwa,”alisema Beng’i.

Aidha, alisema pia katika program hiyo watafufua vitu vya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo hadi kwa sasa kwa nchi nzima vipo 25 na kwa mkoa wa Shinyanga vipo vitatu.

Alisema serikali ina mifuko 72 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, na kwamba mifuko hiyo inatoa mikopo ya riba nafuu.