INEC yawapa angalizo watendaji uboreshaji Daftari la Wapigakura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:38 AM Sep 16 2024
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk.
Picha:Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapigakura kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo, ukiwamo utunzaji vifaa vya uandikishaji.

Wito huo ulitolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk, wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji daftari hilo ngazi  ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Dodoma.

"Vifaa hivi (vya uboreshaji daftari) vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini. Kutokuwa makini katika utunzaji vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu," alionya.

Aliwataka watendaji hao kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na INEC ili wayafanyie kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza. 

Akifungua mafunzo kama hayo mkoani Singida, Mjumbe wa Tume hiyo, Dk. Zakia Mohamed Abubakar, alisema matokeo bora ya zoezi la uboreshaji wa daftari yatatokana yanategemea kuwapo ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

"Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yoyote, msisite kuwasiliana na tume," alisema mjumbe huyo.

INEC pia imewataka mawakala wa vyama vya siasa kutowaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji maboresho ya daftari.

Dk. Zakia alisema wakati wa uboreshaji daftari, mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwapo katika vituo vya kuandikisha wapigakura ili kuleta uwazi katika zoezi hilo.

"Mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika na hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima lakini hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wakitekeleza majukumu yao vituoni," alisema.

Alisema tume ilishatoa kibali kutoa elimu ya mpigakura wakati wa uboreshaji daftari kwa asasi za kiraia 157 na asasi nyingine 33 zitahusika kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo.

Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya mzunguko wa tano wa uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao utajumuisha mkoa wa Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri za Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa, Mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjiro na mkoa wa Singida. 

Uboreshaji wa daftari kwenye maeneo hayo utaanza Septemba 25 hadi Oktoba Mosi mwaka huu na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.