Serikali itumie TFC kumaliza tatizo la bei na usambazaji mbolea nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:11 PM Sep 17 2024
 Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuiwezesha Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) kwa mtaji ili kutatua tatizo la ucheleweshaji wa mbolea na uwepo wa mbolea isiyokuwa na ubora na kukabiliana na kupanda kwa bei ya mbolea nchini. Pia, chama kimeitaka serikali kulipa madeni yote inayodaiwa na kampuni zilizopewa kazi ya kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima.

Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe, akiwa kwenye mkutano wa hadhara Ludewa, mkoani Njombe, jana Septemba 16, 2024. Kiongozi huyo amefafanua na kusisitiza kuwa, ili kukabiliana na changamoto za mbolea katika sekta ya kilimo, Serikali inapaswa iwekeze kwa TFC, ili kampuni hiyo iweze kuwa ya ushindani.

“Chama chetu [ACT Wazalendo] tangu mwaka 2024 tulipigania Kampuni ya mbolea ya Taifa kuongezewa mtaji, kuongezewa nguvu ili iweze kushindana na wauzaji mbolea binafsi, sekta na kampuni binafsi ili kuleta ahueni, kushusha bei ya mbolea na kupata mbolea yenye ubora.” 

Zitto alisisitiza kuwa, “Jambo la mbolea huwezi kuliacha kwenye mikono ya sekta binafsi peke yake. Tunataka sekta binafsi na umma kupitia Kampuni ya Taifa ya Mbolea (TFC) washindane kwenye soko.”

Aidha, Kiongozi wa Chama Mstaafu amemtaka Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha kulipa madeni ya kampuni zilizosambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima ili kuziwezesha kampuni hizo kusambaza mbolea kwa wakati na kupunguza uhaba wa mbolea nchini.

“Tunataka serikali nayo iwajibike. Makampuni yanayouza mbolea inayotolewa kwa ruzuku yanaidai serikali mabilioni ya fedha. Kiasi kwamba makampuni haya yanakula mitaji yao na kushindwa kuleta (kusambaza) mbolea kwa wakati. Nataka niwaambie Waziri wa Kilimo, Ndugu Hussein Bashe, na Waziri wa Fedha, Ndugu Mwigulu Nchemba, walipeni makampuni ya mbolea fedha zao za kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima ili waweze kuleta mbolea kwa wakati.”

Kiongozi Mstaafu alisisitiza kuwa kusuasua kwa mfumo wa usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima kunateteresha uzalishaji na kutishia maendeleo ya taifa. Katika rai yake kwa wananchi, Ndugu Zitto Kabwe, amesisitiza kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitaendelea kuwa mstari wa mbele kupaza sauti ili kuwanusuru wakulima mkoani Njombe, Iringa, Ruvuma na kote nchini; ambao miongoni wao wamekieleza Chama cha ACT Wazalendo kuwa wanakabiliana na uhaba wa upatikanaji wa mbolea; gharama ya mbolea kuwa juu; ucheleweshaji na uwepo wa mbolea ya ruzuku isiyokuwa na ubora, pamoja changamoto nyingine nyingi katika sekta ya kilimo.

Viongozi wakuu wa chama wanaendelea na ziara katika maeneo mbalimbali nchini ambapo leo Kiongozi wa Chama Dorothy Semu atakuwa na Mkutano Rombo (Kilimanjaro) Makamu Mwenyekiti Isihaka Mchinjita atakuwa na Mkutano katika Jimbo la Ubungo (Dar es Salaam) na Kiongozi wa Chama Mstaafu Zitto Zuberi Kabwe atakuwa jimbo la Isimani (Iringa). Ziara hii ni mwendelezo wa kampeni ya kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 na maandalizi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji.