Wizara yatoa angalizo chumvi ya upako

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:57 AM Sep 19 2024
Chumvi.
Picha:Mtandao
Chumvi.

MKURUGENZI Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza - Wizara ya Afya, Dk. Omari Ubuguyu, amesema matumizi holela ya dawa yanayofanywa na baadhi ya watu yanachangia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ambayo tiba zake ni ghali.

Amesisitiza kuwa kitu kinachoathiri zaidi taifa hivi sasa ni magonjwa hayo na kuwaomba viongozi wa dini kubeba ajenda hiyo ili kusaidia kwa kuwa ni rahisi waumini kuwasikiliza kuliko wataalamu wa afya.

Dk. Ubuguyu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya viongozi wa dini kuhusu magonjwa yasiyoambukiza yaliyoandaliwa na Chama cha Wagonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA).

"Kwa wale mnaotoa chumvi, mnatoa maji ya upako, mnatakiwa kukumbuka chochote kinachoingia ndani ya mwili kinatakiwa kifanyiwe kazi na kinachofanya kazi ni figo na ini.

"Wengi ambao wameathirika ni kwa kutumia dawa holela wameathiri ini na figo. Jana nilikuwa Hospitali ya Rufani ya Temeke (Dar es Salaam) kuna binti mwenye umri wa miaka 23 yuko katika huduma za kusafisha figo na huu ni mwezi wa pili ameanza matibabu.

"Ndugu zake wanamchangia, amepata msamaha analipa Sh. 150,000, ameshindwa kwenda hospitalini mara tatu kwa sasa anakwenda mara mbili, itafika atashindwa, atakwenda mara moja.

"Nilitaka kujua nini chanzo cha ugonjwa labda ni shinikizo la damu au kisukari, lakini kumbe ni matumizi holela ya dawa," alisema.

Dk. Ubuguyu alisema binti huyo hajawahi kuumwa sukari wala presha bali alikuwa akiumwa kichwa mara kwa mara, hivyo alikuwa akimeza paracetamol na dawa nyingine ili zimsaidie.

"Ghafla akaanza kuona miguu inavimba, akaanza kupata shida katika upumuaji, akaenda Hospitali ya Temeke, alipopimwa figo zikaonekana zimekufa na sasa anaingia kwenye usafishaji figo, maisha yake yote au apate ndugu wa kumchangia figo," alisema.

Dk. Ubuguyu alisema hiyo ni kutokana na matumizi ya dawa kiholela bila kufuata utaratibu na ushauri wa daktari.

"Dawa za paracetamol zinaathiri figo. Baadhi ya viongozi wa dini wanatoa chumvi wakiwaambia ni upako wakatumie, mwenzako atakwenda kuweka nyingi ili apone na tatizo linakuwa kubwa zaidi, ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya hasa wenye magonjwa," alisisitiza.

Alisema mtu ambaye figo hazifanyi kazi kila baada ya siku moja anakwenda hospitalini kusafisha na kila akienda humgharibu kati ya Sh. 200,000 mpaka Sh. 250,000, kwa wiki Sh. 750,000 na kwa mwezi Sh. milioni tatu.

Dk. Ubuguyu alisema ameamua kusisitizia hilo kwa sababu watu wanaopata magonjwa wengine wanapona, lakini magonjwa hayo yana tabia ya kuwa katika hali ya chini bila kuonesha dalili zozote.

"Ombeeni watu, toeni maji ya upako, wapeni dawa, lakini wakumbusheni kupima afya zao. Mkiwahudumia warudi kupima ili kuangalia ngazi ya matibabu yao, wahimizeni kuzingatia mtindo bora wa maisha," alisema.

Ofisa Habari Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), John Kamoyo, alisema viongozi wa dini wana wajibu wa kuzungumza na waumini namna ambavyo wanaweza kutengeneza maisha yao kwa sababu hata vitabu vya Mungu vinazungumza juu ya afya njema.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Hamisi Mataka, alikumbusha kwamba Uislamu umeweka kanuni kwamba, yeyote ambaye atamtibia mtu bila ya kujua maradhi yake anabeba mzigo wa kitakachotokea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Viongozi wa Dini Mbalimbali kwa Ujenzi wa Amani Tanzania, Mch. Thomas Muyya, alisema wameitikia wito kuhudhuria mafunzo hayo ili kupata elimu na kuichukua kwenda kuwaelimisha Watanzania kupitia nyumba za ibada.

Shujaa wa kisukari aina ya kwanza, Gaudencia Nyeupe, alisema akiwa chuoni, alianza kuona dalili za kisukari na kwa sababu alishaona wagonjwa wa namna hiyo, alichukua hatua ya kupima na kugundulika anacho na sasa anaendelea vizuri kutokana na kufuata masharti anayopewa na wataalamu wa afya.

Samweli Maingu mwenye tatizo la sikoseli, alisema alichelewa kujua kama anaugua ugonjwa huo kwa sababu ya kukosa elimu, lakini alipogundua ameweza kushinda na sasa anaishi maisha ya kawaida huku akiendelea na masomo yake.